Date: 
19-02-2026
Reading: 
Amosi 7:1-6

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 19.02.2026

Amosi 7:1-6

1 Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme.

2 Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo.

3 Bwana akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana.

4 Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukavila vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu.

5 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo.

6 Bwana akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU.

Rarueni mioyo yenu;

Amosi anatabiri hukumu ijayo kwa Israeli kwa maono ya nzige na moto. Amosi anaonesha mimea iliyostawi, lakini ikaliwa na nzige. Ni picha ya Taifa lililoanguka dhambini. Ndiyo maana Amosi anamuuliza Bwana, Yakobo atasimamaje? Anaonesha udhaifu wa mwanadamu pasipo huruma ya Mungu. Hata moto ulipounguza kila kitu, Amosi anamuuliza Bwana Yakobo atasimamaje? 

Nzige na moto vinaangamiza mazao na vitu, lakini Yakobo anaomba Bwana awahurumie watu wake, Bwana anaghairi moto na nzige. Amosi anajenga picha ya Mungu mwenye huruma, anayesamehe. Tunakumbushwa katika majira haya kwamba Mungu wetu ni mwenye kusamehe dhambi. Kumbe tutubu dhambi zetu ili tusamehewe, Kristo awe ndani mwetu daima. Amina

Siku njema

Heri Buberwa