Hii ni Kwaresma
Jumanne asubuhi tarehe 03.03.2026
Waamuzi 16:23-31
23 Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu.
24 Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.
25 Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.
26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.
27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza.
28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.
29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto.
30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.
31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.
Ukatili upo, tuupinge;
Sura ya 16 inahitimisha simulizi ya Samsoni mnadhiri wa Mungu aliyekuwa na nguvu nyingi. Alikuwa amewasumbua wafilisti sana, wakawa wanatafuta jinsi ya kumkamata. Samsoni alimpenda Delila, Wafilisti wakamtumia Delila kufahamu kwa nini Samsoni alikuwa na nguvu. Delila alimshawishi Samsoni mara kadhaa bila mafanikio (inaandikwa mara 3), mara ya nne Samsoni akatoa siri kwamba hakuwahi kunyolewa nywele! Aliponyolewa nguvu zikamuishia, Wafilisti wakamkamata, wakamtoboa macho, wakampeleka gerezani.
Sasa somo linaanzia hapo, Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Mungu wao, Dagoni. Walikula, walikunywa, walifurahi. Samsoni akawekwa katikati yao acheze. Basi Samsoni akamwita Bwana, na kwa msaada wa Bwana akaangusha nyumba ile ambamo sherehe ilikuwa inafanyika. Walikufa Wafilisti wengi sana. Samsoni alifanyiwa ukatili toka anakamatwa, kutobolewa macho, kufungwa gerezani na kazi ngumu. Lakini alihitimisha kwa ushindi mkubwa, Wafilisti wakifa wengi na Mungu wao Dagoni. Tuendelee kukumbuka daima kwamba ni Mungu pekee astahiliye kuabudiwa, na nguvu za Mungu ziko juu ya vyote. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
