Date: 
25-04-2025
Reading: 
Marko 16:12-13

Hii ni Pasaka

Ijumaa asubuhi tarehe 25.04.2025

Marko 16:12-13

12 Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba.

13 Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.

Tembea na Yesu mfufuka;

Injili ya Marko huandika kwa ufupi sana kuhusu kufufuka na kupaa kwa Yesu. Sura ya 16 pekee ambayo ni ya mwisho huandika juu ya kufufuka kwa Yesu, kuwatokea mitume/mariamu na wengineo, na kupaa. Kwa ufupi huo huo, asubuhi ya leo tunaona akiwatokea watu wawili waliokuwa wakielekea shambani. Hawa aliwatokea wakamtambua lakini Marko anasema walipeleka habari lakini hawakuwaamini.

Marko kama kawaida yake ya kuandika kwa ufupi, anaandika habari kwa mistari miwili. Lakini Luka anaandika kwa kirefu, habari hii ambayo inawahusu watu wawili waliokuwa wakielekea Emau

(Luka 24:13-35). Wawili hawa walikuwa wakitembea kuelekea Emau na kujadili yaliyotokea. Yesu akaungana nao wasimtambue. Akawauliza mnaongea nini? Wakamshangaa wakimuuliza kama ni mgeni Yerusalemu. Wakamsimulia yote yaliyotokea kuhusu Yesu aliyekuwa anafundisha na kuhubiri, jinsi alivyoteswa akauawa na kuzikwa, na sasa amefufuka

Yesu akaanza kuwasimulia habari za ukombozi toka enzi za Musa na manabii. Akasema ilimpasa kufa watu wakombolewe. Akaendelea kuwaambia kuwa mioyo yao mizito kuamini yote ya manabii na Yesu mwenyewe. Walipokaribia Emau wakaomba Yesu akae nao, akakaa nao chakulani na kumega mkate, akabariki na kuwapa, wakamtambua. Luka anasimulia hivi

Hapa ndipo Marko anasema wakarudi kuwapa wengine habari, japo wengine hawakuwaamini. Wale ndugu wawili walimtambua Yesu, wakamwamini. Nasi tunaalikwa kudumu katika Kristo, tutembee na Yesu mfufuka. Amina

Ijumaa njema

 

Heri Buberwa