Date: 
28-04-2025
Reading: 
Kutoka 15:22-26

Hii ni Pasaka

Jumatatu asubuhi tarehe 28.04.2025

Kutoka 15:22-26

22 Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

24 Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;

26 akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

Yesu ajifunua kwetu;

Mungu aliwakomboa wana wa Israeli toka kifungoni kwa mkono wake. Nguvu yake na uwezo ilidhihirika walipotembea juu ya nchi kavu katikati ya bahari. Maji yalipoungana tena majeshi ya Misri wakaangamia, ilikuwa ni maafa! Israeli waliangalia nyuma na kuona majeshi waliokufa, wakamcha na kumwamini Bwana;

Kutoka 14:31

Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya Bwana juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha Bwana, wakamwamini Bwana, na Musa mtumishi wake.

Baada ya kuvuka kuvuka bahari nyekundu, waliimba wimbo wa kwanza ulioandikwa kwenye Biblia takatifu (Kutoka 15). Ukisoma sura ya 15 unaona jinsi ambavyo wimbo huu ulileta furaha katika Bwana (Soma Kutoka 15:1-19). Kama tulivyosoma kwenye somo, siku tatu baadaye watu wakaanza kumnung'unikia Musa, baada ya kukosa maji. Walipofika sehemu iitwayo Mara wakapata maji lakini machungu! Manung'uniko yao kwa Musa ukweli yalikuwa yanamuelekea Mungu. Na kilichofanya wanung'unike, macho yao hayakuwa kwa Bwana tena.

Musa alimlilia Bwana (25) na Mungu akamwonyesha mti alioutia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Mungu alifanya lililo sahihi kwa Israeli, akawaambia kuisikia sauti yake na kutii amri zake. Kwa mawazo yangu hakuna muujiza hapa, bali Mungu anajibu sala ya Musa (25). Mti uliotupwa kwenye maji ilikuwa alama au ishara ya Mungu kuwa muweza. Hakukuwa na muujiza wowote kwenye mti, bali ni nguvu ya Mungu iliyotibu maji, hadi Israeli kukiri kumuona Bwana!

Mwishoni wa somo (26) Bwana anajidhihirisha kama mponyaji. Hapa ifahamike kuwa Bwana siyo mponyaji wa mwili tu, bali roho za watu. Mungu alikuwa akionesha ukuu wake kuwa yeye ndiye mponyaji. Hakuwaponya Israeli kwa kuwapa maji tu, bali alikuwa mponyaji wao kiroho wasiangamie. 

Yesu Kristo mponyaji;

Tunaposoma uponyaji leo katika Agano la kale, tunamsoma Yesu mwenyewe. Alipoanza kazi yake, alisoma hekaluni kilichomleta akimnukuu Isaya;

Luka 4:18-19

18 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,
19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.

Kwa muda wa miaka mitatu Yesu alihuhiri, alifundisha na kuponya. Alisamehe dhambi. Popote alipopita, na wote walioletwa kwake waliponywa. Pamoja na maswali mengi toka kwa Mafarisayo, Yesu hakuacha kuponya na kusamehe dhambi.

Sasa basi;

Kwa mujibu wa somo letu, Yesu ni vyote viwili, yaani mti na maji. Alibeba dhambi zetu msalabani ili tukahesabiwe haki, na kwa kupigwa kwake tuliponywa;

1 Petro 2:24

Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.

Yesu pekee huleta uponyaji wa kiroho kwa waliokata tamaa. Ni maji machungu yanakuwa matamu. Alikufa msalabani tukapona.

Msalaba ni mti, dhambi zetu ni maji machungu. Msalabani alibeba dhambi zetu sisi tukapona, yaani kwa njia ya msalaba tumeokolewa. Hivyo kwa njia ya msalaba tumesamehewa dhambi zetu. Huyu ndiye Yesu Kristo aliye mwingi wa huruma na haki.

Nakualika kutafakari njia zako sasa unapoendelea kuishi kwa neema ya Mungu. Maji yako machungu au matamu? Umesamehewa dhambi zako au bado? Yaani umempokea Yesu? Utazame msalaba (mti) ili unywe maji matamu (uokolewe)

Tafakari ukuu wa Bwana kwa kumfuata, maana alimaliza kazi msalabani kwa ajili yako.

Nakuacha na swali;

Maji yako matamu au machungu?

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com