Hii ni Pasaka
Jumanne asubuhi tarehe 29.04.2025
Yoshua 3:9-17
9 Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu.
10 Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi.
11 Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani.
12 Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja.
13 Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu.
14 Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la agano wakatangulia mbele ya watu,
15 basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno),
16 ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko.
17 Na hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hata taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.
Yesu ajifunua kwetu;
Baada ya Yoshua kupewa maelekezo na Bwana kuhusu sanduku la Agano, Yoshua anawaita watu kuyasikia maneno ya Bwana. Kwa kumsikia Bwana Yoshua anawaambia watamjua Mungu aliye hai. Yalikuwa ni maelekezo jinsi ya kuvuka Yordani wakiwa na sanduku la Agano. Walimsikiliza Yoshua, wakapata kuvuka Yordani wakiwa na sanduku la Agano.
Mungu alikuwa anawasiliana na wana wa Israeli kupitia kwa Yoshua kama tulivyoona. Asubuhi hii Mungu anaongea nasi kwa njia ya neno lake. Kwa maudhui ya juma hili, naweza kusema Yesu anajifunua kwetu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Kufufuka kwake ni ushindi kwetu, hivyo tumwamini daima. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa