Date: 
26-05-2025
Reading: 
Luka 11:5-8

Hii ni Pasaka;

Jumatatu asubuhi tarehe 26.05.2025

Luka 11:5-8

[5]Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,

[6]kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;

[7]na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?

[8]Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

Ndugu wakae pamoja kwa umoja;

Katika somo tulilosoma;

Tunaona ni wakati wanafunzi walipomuomba Bwana Yesu awafundishe kuomba. Anaanza kuwafundisha kwa njia ya swali lenye vipengele vingi.

1.Yesu anaanza na mtu anayeenda kwa rafiki yake usiku wa manane.

Usiku wa manane huwa ni muda ambao watu wamepumzika, wengi wamelala fofofo. Kama ni giza, litakuwa ni giza totoro.

Tafsiri ya "usiku" ni kuwa tuombe wakati "wowote". Huyu mwenye shida hasubiri kupambazuke! Na sisi tusiombe tunapojisikia, tuombe wakati wote. Tupeleke haja zetu mbele za Mungu wakati wowote, yuko tayari kusikia kuomba kwetu. 

2.Mmoja anapogonga na kutoa haja zake, yupo anayeamka kumsikiliza.

Amelala usiku, lakini anaamka usiku wa manane kumsikiliza rafiki yake. 

Hapa Yesu alikuwa anaelezea kwa njia ya swali, kuwa muda wowote, Mungu yuko tayari kutusikiliza. Kama sisi wenyewe tunasikilizana na kusaidiana, hata usiku wa manane, iweje kwa Mungu aliyetuumba?

Mungu anasikia kuomba kwetu muda wowote.

3.Anayeombwa usiku anampa mwombaji kadri ya haja yake. 

Mungu anasikia kuomba kwetu, na anatujibu kadri ya mapenzi yake. 

4.Lakini pia katika somo la asubuhi ya leo, tunamuona anayeomba usiku kwa rafiki haachi kuomba.

Na huu ndio msingi wa somo la leo asubuhi. Kwamba " tuombe bila kukoma"

Mungu yuko tayari kusikia maombi yetu.

5.Anayemwendea rafiki yake usiku kuomba mkate, na aombwaye akakubali kumpa mwenzake mkate, ni picha ya ndugu wanaokaa pamoja kwa umoja. Itukumbushe nasi kukaa pamoja kwa umoja. 

Uwe na wiki njema. Amina

 

Heri Buberwa Nteboya