Alhamisi, tarehe29.05.2025
Siku ya kukumbuka kupaa kwa Yesu Kristo;
Masomo;
Zab 47:1-9
Rum 8:34
*Yn 16:28-33
Yohana 16:28-33
28 Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.
29 Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote.
30 Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.
31 Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa?
32 Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami.
33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.
Kristo amepaa katika Utukufu wake;
Ni mafundisho ya mwisho ya Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya kusulibiwa, wanafunzi ambao walielekea kuanguka kiroho. Mstari wa 32 unaonesha kuwa wanafunzi walielekea kutawanyika. Walikuwa bado katika tafakari. Muda mfupi uliopita Petro alikuwa amesema yuko tayari kufa, lakini Yesu akamwambia kuwa angemkana mara tatu kabla ya jogoo kuwika (Yoh 13:37-38).
Mstari wa 29 na 30 inaonesha kuwa wanafunzi walianza kuelewa, ili hali Yesu akijua ambayo yangetokea. Lakini Yesu anawaambia kuwa kushindwa kwao kiroho kusingekuwa mwisho wao, akiwataka kushinda majaribu wakimtumikia. Mstari wa 33 unawatia moyo, kuwa pamoja na dhiki waliyonayo wajipe moyo maana Yesu ameushinda ulimwengu. Hivyo leo tunakumbushwa kuwa kwa Yesu aliyeushinda ulimwengu, sisi tunaweza kushinda. Kwa muktadha halisi, tuangalie tunawezaje kushinda na kudumu katika ufalme wa Mungu, kwa kuanzia mistari nyuma ya somo la leo, na baadaye tutaona mkazo katika mistari lengwa ya leo.
Tunashindaje?
1.Lipo tumaini katika Kristo;
Katika somo hilihili ukisoma nyuma mstari wa 25 unaona Yesu akiwaambia wanafunzi kuwa asingesema kwa Mithali tena, bali angewapa habari za Mungu waziwazi. Bila shaka hapa alimaanisha mambo aliyosema nao wakati alipokuwa nao faragha, na bila shaka yote aliyosema nao kwa takribani miaka mitatu. Lugha ya Mithali imetumika pia kwa Yohana 10:6 ikimaanisha maana ambayo siyo ya moja kwa moja bali yahitaji tafakuri. Hivyo wakati huu alilenga kuwa habari moja kwa moja. Na ndiyo maana wanafunzi wanalitambua hilo, ndiyo mstari unaoanza leo;
Yohana 16:29
Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote.Wanafunzi walitambua hivyo, maana alianza kusema nao wakimwelewa yampasayo kuhusu mateso yake, kufa na kufufuka. Zipo sehemu kadhaa ambazo wanafunzi hawakumwelewa Yesu, mfano alipowaosha miguu Petro akakataa, Yesu akiwaambia wangeelewa baadaye (Yoh 13:7)
Katika somo la leo, Yesu alifungua fahamu za wanafunzi wake ili kuwatia moyo katika safari ya utume, hata kama asingekuwepo. Ndiyo maana aliwaambia "Jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu". Anawapa tumaini. Hivyo nasi tuwe na tumaini katika wito wetu kuwa Mungu yu pamoja nasi.
2.Dumu katika Sala;
Yesu aliwaambia mara kadhaa wanafunzi kuomba. Lakini pia katika somo la leo, ukianzia nyuma kidogo mstari wa 26 anawaambia waombe kwa jina lake; "Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba" (Yoh 16:26)
Yesu hakumaanisha kwamba Baba angekuwa mbali nao, bali wangemwomba Baba kwa jina la Yesu, yaani kwa Mungu yule yule mmoja. Kumwendea Baba kupo kwa kazi iliyomalizwa na Yesu msalabani kwa ajili yetu. Kuomba katika jina la Yesu ni kumwendea Mungu kwa msingi wa kazi ya Yesu ambaye kwa njia ya kifo chake ametuingiza katika ufalme wa Mungu. Kushindwa kiroho huambatana na mambo mengi ikiwemo kutofanya sala. Tusichoke, tusali bila kuchoka. Yesu anatuhimiza kuomba kwa jina lake ili tudumu katika ufalme wake.
3.Mungu amejaa upendo na neema;
Katika kuwatia moyo, Yesu alionesha kuwapenda sana. Ndiyo maana anaonesha upendo wake (27). Upendo wake ni mkubwa kuliko wetu kwake, maandiko huthibitisha;
1 Yohana 4:10
Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.Upendo wa Mungu ni dhahiri. Upo mstari maarufu sana (Yoh 3:16) kwamba Mungu aliupenda ulimwengu akamtoa mwana wake wa pekee. Kumbe, wito wa kuingia katika ufalme wake tunapewa kwa upendo mkuu utokao mbinguni. Uko tayari kupoteza fursa hii?
4.Anayetuita kwenye ufalme, ndiye anayemiliki ulimwengu;
Ukweli huu unakuja mwanzoni kabisa mwa somo la leo;
Yohana 16:28
Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.Yesu alikuja duniani kama mwanadamu akiwa Mungu kweli. Na baada ya kazi yake alipaa kurudi mbinguni kwa Baba yake.
Kazi yake aliimaliza. Asingeimaliza asingeruhusiwa kurudi mbinguni. Yote hii ilikuwa ni mpango wa kutuingiza katika ufalme wa Mungu. Hivyo wokovu wetu hautegemei ukamilifu wetu, bali neema ya yeye anayemiliki dunia hii. Tukipata wokovu huu, tunaingia katika ufalme wa Mungu.
5.Amani yetu iko kwa Kristo, na siyo kwa kazi zetu;
Hapa ndipo kuna mkazo wa somo la leo;
Binafsi nafikiri wanafunzi walifikiri wameanza kumuelewa Yesu, lakini Yesu akawapa changamoto;
Yohana 16:31
Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa?Anawahoji kuhusu kuelewa kwao. Yesu aligundua bado kuna kitu walikuwa hawajaelewa, anawaambia kuwa watatawanyika (32). Na kwa sababu hiyo, anawaambia wawe na amani maana yeye ameushinda ulimwengu (33).
Yesu alikuwa akifanya uponyaji, alimtakia amani aliyeponywa;
Luka 7:50
Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.Luka 8:48
Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani.Tafsiri yake ni kuwa Yesu hutuombea kuwa na amani siku zote. Lakini pia, Yesu alituachia amani;
Yohana 14:27
Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.Kristo amepaa katika Utukufu wake;
Somo la Alhamisi ya leo linatuonesha Yesu akiongea na wanafunzi wake kabla ya kusulibiwa. Katika neno tulilosoma, Yesu anamaliza kuwatia moyo, kwamba wawe na amani, ulimwenguni wanayo dhiki lakini yeye (Yesu) ameushinda Ulimwengu. Faraja hiyo aliyowapa wanafunzi, ndiyo nasi tunapewa leo, kwamba tuwe na amani, Yesu ameushinda ulimwengu. Baada ya Yesu kusulibiwa, alipaa kurudi mbinguni. Kupaa kwake kuliashiria nini?
1. Kupaa kwa Yesu kuliashiria kuhitimisha kazi yake hapa duniani
2. Kupaa kwa Yesu kuliashiria kuanza kwa huduma yake mbinguni
3. kupaa kwa Yesu kuliashiria kuanza kwa huduma yetu kama wawakilishi wake hapa duniani
Mwisho;
Kama tunavyokiri katika ukiri wa Imani;
"Siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu, akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba Mwenyezi, kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu..."
Tuadhimishe na kukumbuka kupaa kwa Yesu tukijua kuwa Yesu atarudi tena. Hivyo tunawajibika kujiandaa ili Yesu akirudi tusiachwe. Usifadhaike
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650