Date: 
02-12-2025
Reading: 
Isaya 61:6-9

Hii ni Advent;

Jumanne asubuhi tarehe 02.12.2025

Isaya 61:6-9

[6]Bali ninyi mtaitwa makuhani wa BWANA; watu watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao.

[7]Badala ya aibu yenu mtapata maradufu, na badala ya fedheha wataifurahia sehemu yao; basi katika nchi yao watamiliki maradufu; furaha yao itakuwa ya milele.

[8]Maana mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele.

[9]Na kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa na BWANA.

Bwana mwenye haki analijia Kanisa lake;

Somo la asubuhi ya leo linahusu habari njema ya ukombozi, maana mwanzoni (61:1) Isaya alitabiri ujio wa Yesu miaka 700 kabla. Katika utabiri huo, Isaya alionesha urejesho na tumaini katikati ya Taifa la Mungu. Israeli walikuwa wamevunja Agano la Mungu, hivyo Isaya akatabiri watu kupelekwa Babeli uhamishoni na Yerusalemu kuharibiwa.  

Ilikuwa ni taswira ya Mungu katika kuchukia uovu. Lakini Isaya anaonesha tumaini lisilokoma, pale anapotabiri neema ya Mungu kwa watu wake. Katika tumaini hilo, Isaya anatabiri Ujio wa Yesu Kristo, utabiri ambao Yesu Kristo alikuja kuurejea baadaye kwenye Agano jipya, yaani Yesu anairejea Isaya 61:1 anaposoma;

Luka 4:18

[18]Roho wa Bwana yu juu yangu, 
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. 
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, 
Na vipofu kupata kuona tena, 
Kuwaacha huru waliosetwa,

Yesu ndiye alikuwa utimilifu wa unabii wa Isaya kama alivyodhihirisha mwenyewe hekaluni. Hili linaonekana katika mstari wa tatu, Isaya anapotabiri furaha kwa Taifa la Mungu badala ya maombolezo. Yesu ndiye alikuja kuleta furaha hii, kwa kuwaondolea watu dhambi zilizowatenganisha na Mungu. Ni katika kuleta msamaha huo, Taifa la Mungu linaahidiwa kuumiliki ulimwengu (5)

Utangulizi huo unatuleta kwenye somo la asubuhi ya leo;

Sisi ni makuhani;

Katikati ya Taifa lililoharibiwa, Isaya anatabiri ukombozi na watu wa Mungu kuitwa makuhani. Kwa nini Isaya anatumia picha ya ukuhani?

Chini ya sheria ya Musa, makuhani walitolewa kwenye kazi nyingine kwa sababu wao walipewa kumtumikia Bwana tu. Kabila la Lawi waliitenda kazi ya Mungu, wakati makabila yote ya Israeli yaliyobaki walifanya kazi ya shamba (ardhi). Hii ndiyo picha ya sisi tulio wafuasi wa Kristo. Tumetengwa kufanya kazi kama makuhani wa Mungu. 

Katika historia ya ukuhani katika Israeli, lengo la ukuhani lilikuwa kumtumikia Mungu na kuwahudumia watu wa Israeli. Kuhani alihudumu kati ya Mungu na wanadamu. Kuhani alitakiwa kujua sheria za Mungu na kuwafundisha watu. Kumbe nasi tunaalikwa kupeleka maarifa ya kiMungu kwa watu, ili kuujenga ufalme wa Mungu. Makuhani walitakiwa kuwaleta watu kwa Mungu. Ni njia aliitumia Mungu kueneza ufalme wake. 

Katika Agano jipya, kazi ya ukuhani inaletwa kwa kundi la waaminio, yaani sote ni makuhani;

1 Petro 2:9

[9]Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;

Tunayo mamlaka ya kikuhani, chini ya Yesu Kristo aliye kuhani mkuu tunayemwabudu. 

Katika Biblia baraka hutoka kwa njia tatu;

Mungu kwenda kwa watu

Watu kwenda kwa Mungu

Watu kwenda kwa watu

Kwa sababu Yesu yuko ndani yetu, tunayo nafasi ya kuwa baraka miongoni mwetu, sisi kwa sisi. 

Kwa maana hiyo, maisha yetu lazima yamwakilishe Yesu kwa wengine. 

Hivyo basi; ujio wa Yesu ulikuwa ni kuleta ufalme wake, ambao tunaalikwa kuutangaza kwa kazi zetu. Kama alivyotabiriwa akaja, akarudi kwa Baba, atarudi tena kwa Utukufu wake ambapo tutawajibika kwa matendo yetu. Tuutumie ukuhani tuliopewa kumcha Bwana na kuwaleta wengi kwa Yesu ili akirudi asimuache hata mmoja.

Mwisho;

Tunaishi katika dunia inayohitaji urejesho.

Sisi ni wenye dhambi ambao;

-Hatujaitwa tu kuhudhuria ibada

-Kushiriki meza ya Bwana ya tu hakutoshi (simaanishi usishiriki)

-hatujaitwa tu kutoa sadaka nyingi n.k

Yote hayo na mengine yatufanyayo kuwa washirika katika Kristo, lazima tuyafanye kwa utukufu wa Mungu, kwa maana sisi tupo kwa ajili ya Utukufu wa Mungu. Tuandae mioyo yetu kumpokea Kristo, na kama makuhani tuwape wengine habari za Yesu tunayemngojea. 

Yesu alikuja, Yesu hukaa kwetu, na pia atarudi tena kwa mara ya pili katika Utukufu wake. Ndiyo maana leo tunakumbushwa kuwa Bwana anakuja, tuandae mioyo yetu.

Jumanne njema.

 

Heri Buberwa Nteboya  

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com