Jumatatu asubuhi tarehe 05.01.2026
Mwanzo 17:1-8
1 Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu.
2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.
3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema,
4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi,
5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.
6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako.
7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.
8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.
Utukufu wa Mungu umefunuliwa katika Yesu Kristo;
Asubuhi ya leo tunasoma juu ya ishara ya Agano la Mungu kwa Abramu. Mungu anamuita Abramu na kumuambia awe mkamilifu, anampa agano la kumzidisha. Mungu anaendelea kumwambia Abramu kuwa atakuwa baba wa wa mataifa mengi, na hataitwa Abramu tena, bali Ibrahimu. Ibrahimu anaahidiwa uzao mwingi sana, na wafalme wengi kutoka kwake. Agano hili ni la milele kwa Ibrahimu na uzao wake wote. Mwisho wa somo anaahidiwa kupewa nchi yote ya Kanaani, na muhimu kabisa, Bwana anaahidi kuwa Mungu wake Ibrahimu.
Kwa agano tunaloliona hapo juu, Ibrahimu alikuwa Taifa kubwa, akatoa wafalme wengi, yaani agano la Mungu lilitimia. Agano la Mungu kwetu ni wokovu kwa njia ya Yesu Kristo, ambapo kila aaminiye huokolewa. Yesu alitabiriwa na manabii, na Yesu alikuja akazaliwa duniani. Huu ulikuwa utimilifu wa agano la Mungu juu ya wokovu wetu, tuliokolewa kama alivyoahidi. Basi tudumu katika Kristo, ili utukufu wa Mungu uonekane katika Kristo. Nakutakia mwaka mpya wenye mafanikio. Amina
Heri Buberwa Nteboya
Mlutheri
