Date: 
13-01-2026
Reading: 
Waefeso 3:1-12

Hii ni Epifania 

Jumanne asubuhi tarehe 13.01.2026

Waefeso 3:1-12

1 Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa;

2 ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu;

3 ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache.

4 Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6 ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;

7 Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.

8 Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;

9 na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote;

10 ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;

11 kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.

12 Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

Ubatizo wetu;

Mtume Paulo anawaandikia Waefeso juu ya huduma yake kwa mataifa, kwamba yeye ni mfungwa wake Kristo kwa ajili ya hao mataifa. Anasema alifunuliwa siri za Kristo, ili watu wapate ufahamu na kumwamini huyo Kristo. Paulo anaendelea kusema kuwa yeye ni mhudumu wa Injili, kwa kipawa alichokipewa kwa neema ya Mungu. Paulo anajiona mdogo katika wote, lakini aliyepewa neema ya kuhubiri Injili.

Msisitizo wa Paulo ni kusudi la Mungu, kwamba Injili ihubiriwe na watu wote waokolewe. Paulo anauonesha ujasiri alio nao katika kazi ya Injili, akitukumbusha wajibu na nafasi zetu katika kazi ya Injili. Tunao wajibu wa kuihubiri Injili kwa watu wote. Maisha yetu ni mahubiri tosha, ikiwa tutaiishi ahadi ya ubatizo wetu. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri