Event Date: 
30-09-2022

Jumapili ya tarehe 18/09/2022 ilifanyika ibada ya kuwaingiza kazini Wazee wa Kanisa pamoja na Viongozi wa Vikundi waliochaguliwa hivi karibuni katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral. Safu mpya ya uongozi itahudumu katika Usharika wa Kanisa Kuu kwa kipindi cha miaka minne (2022-2026).

Akiongoza ibada ya kuwaingiza kazini watumishi hao wapya, Baba Askofu wa K.K.K.T. Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliwapongeza Wazee wa kanisa pamoja na viongozi wa vikundi waliochaguliwa kwa kuaminiwa na washarika na kuwatakia kila la kheri katika kutimiza majukumu yao kwa maslahi mapana ya usharika na kanisa kwa ujumla.

“Maisha ya Mzee wa Kanisa yana madai, unajua mzee wa kanisa kimsingi ni Msaidizi wa Mchungaji. Kama nyumbani kwako unaishi na Mzee wa Kanisa maana yake unaishi na Msaidizi wa Mchungaji. Kwa upande wa vikundi, tunataka vikundi viwe karibu na Mungu. Wewe ambaye upo katika kikundi, kikundi kionekane kinabadilika. Sisi ndio nuru kwenye maeneo tunayoyaongoza, tuendeleze pale ambapo wenzetu wameishia,” alisema Baba Askofu.

Baba Askofu Dk. Alex Malasusa akizungumza wakati wa ibada

Katika hatua nyingine, Wazee wa Kanisa na Viongozi wa Vikundi waliomaliza muda wao (2018-2022) waliagwa na Usharika wa Kanisa Kuu na kupongezwa kwa utumishi wao uliotukuka kwa kipindi chote ambacho walihudumu katika Usharika wa Azania Front Cathedral.

Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliwapongeza watumishi hao waliomaliza muda wao kwa kumtumikia Mungu katika kipindi chao chote cha utumishi na kuwasihi kuendelea kutoa mchango wao kwa uongozi mpya ili uweza kufanikisha malengo ya usharika na kanisa kwa ujumla.

“Sehemu alipo Mzee wa Kanisa inabidi iwe ni sehemu yenye manukato. Wewe ambaye ulikuwa ni mzee wa Kanisa potelea mbali hata kama ni kwa siku mbili, wewe ni chumvi. Hifadhi pale palipokuwa panaharibika. Mmepumzika kuhudhuria vikao na mikutano ya usharika lakini utumishi wenu hauna mwisho,” alisema Baba Askofu.

Kwa upande wake; Profesa Charles Mkonyi akizungumza kwa niaba ya Wazee wa Kanisa waliomaliza muda wao aliwashukuru washarika kwa kuwapa ushirikiano kwa kipndi chote cha utumishi wao. “Tunamshukuru Mungu aliyetupa uhai na fursa ya kutumika katika shamba lake, sifa na utukufu tunarudisha kwake.”

Ibada hiyo maalum pia ilihudhuriwa na Msaidizi wa Askofu Dean Chediel Lwiza pamoja na Mchungaji Kiongozi wa Usharika, Chaplain Charles Mzinga.

Baba Askofu Dk Alex Malasusa, Chaplain Charles Mzinga na Dean Chediel Lwiza wakati wakiingia kanisani kwa ajili ya kushiriki ibada.

Sehemu ya washarika wakifuatilia ibada

Shukrani kwa viongozi wa vikundi (pichani) waliomaliza muda wao wa utumishi

Vyeti vya shukrani kwa wazee wa kanisa waliomaliza muda wao wa utumsihi (2018-2022)

Picha ya pamoja ya wazee wa kanisa waliomaliza muda wao wa utumsihi (2018-2022)

Mkono wa Baraka kutoka kwa Baba Askofu 

Baadhi ya wazee wa kanisa walioingizwa kazini baada ya kuchaguliwa hivi karibuni. Watahudumu kwa kipindi cha miaka minne (2022-2026).