Date: 
02-11-2022
Reading: 
2Wafalme 23:1-3

Jumatano asubuhi 02.11.2022

2 Wafalme 23:1-3

[1]Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.

[2]Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA.

[3]Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.

Ushuhuda wetu; Hapa nimesimama;

Mfalme Yosia akiwa anatawala, watumishi wake kuna wakati walifanya mambo yasiyofaa, hadi Mfalme akaletewa ujumbe huu;

2 Wafalme 22:16-17

[16]BWANA asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda;
[17]kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike.

Somo la asubuhi hii tunasoma Yosia Mfalme akifanya matengenezo. Anapanda hekaluni na kufanya Agano na Bwana la kufuata maagizo na shuhuda zake. Na watu wote walikubali Agano hilo.

Tunaalikwa kuishi maisha ya matengenezo kila siku. Ni wajibu wetu kumfuata Kristo katika ukamilifu tukiisimamia kweli ya neno lake, ili neema ya matengenezo isiondoke kwetu.

Uwe na Jumatano njema.