Date: 
25-08-2022
Reading: 
Mwanzo 6:12-22

Alhamisi asubuhi tarehe 25.08.2022

Mwanzo 6:12-22

[12]Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.

[13]Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.

[14]Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami.

[15]Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake.

[16]Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu.

[17]Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa.

[18]Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe.

[19]Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke.

[20]Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi.

[21]Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao.

[22]Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.

Tutumie vizuri nafasi tuliyopewa;

Baada ya wanadamu kuwa waovu juu ya nchi, Mungu alimwagiza Nuhu aliyekuwa mwenye haki kutengeneza Safina, ambayo angeingia yeye na wanawe ili asiangamie kwa gharika. Nuhu alikuwa mtii, akatengeneza Safina ambayo aliingia yeye na familia yake. Hata gharika ilipokuja, walikufa wote wenye mwili na wanyama. Walipona tu waliokuwa ndani ya safina.

Funzo;

-Nuhu alikuwa mwenye haki, ndiyo maana Mungu hakumwangamiza. Kwa maana hiyo, maisha yetu yamebeba hatma yetu. Njia zako zitaamua hatma yako.

- Nuhu alipoambiwa kutengeneza safina alitii mara moja. Alitumia nafasi yake kufanya hivyo ambayo ilimsaidia asiangamie. Maisha ya ukristo yanatutaka kuwa watii wa neno la Mungu na kutenda inavyostahili kwa ajili ya uzima wetu.

Tumia vizuri nafasi uliyopewa.

Siku njema