Date: 
18-04-2023
Reading: 
Mwanzo 18:1-5

Hii ni Pasaka

Jumanne asubuhi tarehe 18.04.2023

Mwanzo 18:1-5

1 Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.

2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,

3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.

4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.

5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.

Yesu Kristo ajifunua kwa wanafunzi wake;

Katika sura hii ya 18, ujumbe wa Bwana unakuja katika nyumba ya Ibrahimu. Ibrahimu aliona watu watatu wamesimama mbele yake, akakimbia kuwalaki. Aliwakarimu nyumbani mwake. Ukiendelea kusoma unaona kuwa ndiyo wakati ambapo Ibrahimu aliletewa habari ya kupata mtoto, jambo ambalo Sara alilitilia mashaka, lakini Bwana akakazia kwamba itawezekana maana hakuna jambo linaloweza kumshinda Bwana.

Tunalojifunza asubuhi ni utayari wa Ibrahimu kuupokea ujumbe wa Bwana. Alipokea ujumbe wa Bwana kwa unyenyekevu. Nasi tunaalikwa kuupokea ujumbe wa kufufuka kwa Yesu kwa furaha na unyenyekevu maana kwa Yesu kushinda mauti tumekombolewa. Mungu alimtokea Ibrahimu kwa njia ya malaika wake. Sisi leo Mungu anatutokea kwa njia ya Kristo anayejifunua kwetu kama Bwana na Mwokozi wetu. Mwamini yeye uokolewe.

Siku njema.

Heri Buberwa