Date: 
29-04-2023
Reading: 
Yeremia 50:6-8

Hii ni Pasaka 

Jumamosi asubuhi tarehe 29.04.2023

Yeremia 50:6-8

6 Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.

7 Watu wote waliowaona wamewala; na adui zao walisema, Sisi hatuna hatia, kwa kuwa hao wametenda dhambi juu ya Bwana, aliye kao la haki, yaani, Bwana, tumaini la baba zao.

8 Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi.

Yesu Kristo ni Mchungaji mwema;

Sauti ya Nabii Yeremia inatoa ujumbe juu ya watu (kondoo) wa Mungu waliopotezwa na wachungaji wao. Yeremia alionesha Bwana kuchukia watu wake kupotezwa na kuangukia mikononi mwa adui. Lakini ahadi ya kuwaokoa kondoo waliopotea ipo;

Yeremia 50:19

Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.

Mungu hapendi watu wake wapotee. Tunapokuwa tumepotea Mungu anahuzunika. Yeye hutaka wote watubu dhambi zao.

2 Petro 3:9

Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.

Tumkaribie Yesu kwa imani na toba, ili tuurithi ufalme wake.

Jumamosi njema.

 

Heri Buberwa