Date: 
18-08-2022
Reading: 
2 Timotheo 3:1-9

Alhamisi asubuhi tarehe 18.08.2022

2 Timotheo 3:1-9

[1]Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

[2]Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

[4]wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

[5]wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

[6]Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi;

[7]wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.

[8]Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.

[9]Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri.

Hekima ituingizayo mbinguni;

Mtume Paulo anamwandikia Timotheo juu ya uovu katika siku za mwisho. Paulo anaonesha kuwa zitakuwa siku za hatari. Kwamba watu watakuwa wenye kupenda fedha, kujipenda wenyewe, kujisifu, wenye kiburi, wasio na upendo n.k Ukiangalia na kusoma zaidi unaona Mtume Paulo alimaanisha kwamba kutakuwa na watu wasiomcha Mungu, hivyo akimuandikia Timotheo ujumbe huu kwa ajili yake na Kanisa kwa ujumla.

Mambo aliyoyaandika Mtume Paulo kwenye somo la leo asubuhi ndiyo yaliyopo. Uovu uko kila mahali. Na kwa sababu ya Teknolojia unatambulika kwa urahisi. Kinachosikitisha zaidi, uovu unapewa nafasi kubwa sana kwenye mazingira yetu kuliko mambo mema! Jambo hili liko wazi hasa kwenye mitandao ya kijamii. Sisemi tuiache mitandao ya kijamii maana hilo haliepukiki kwa sasa, bali tuitumie kwa Utukufu wa Mungu tukiepuka uovu. Katika nyakati hizi tuuepuke uovu kwa hekima ya Mungu ndipo tutaingia mbinguni.

Siku njema