Date: 
17-04-2023
Reading: 
Daniel 2:17-24

Hii ni Pasaka

Jumatatu asubuhi tarehe 17.04.2023

Danieli 2:17-24

17 Ndipo Danielii akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake;

18 ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danielii na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.

19 Ndipo Danielii alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danielii akamhimidi Mungu wa mbinguni.

20 Danielii akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake.

21 Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa;

22 yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake.

23 Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme.

24 Basi Danielii akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonyesha mfalme ile tafsiri.

Yesu Kristo ajifunua kwa wanafunzi wake;

Sura ya 2 ikisomwa kuanzia mwanzoni, Nebukadreza aliota ndoto ambayo hakufahamu maana yake. Aliwatafuta waganga, wachawi na wote wenye hekima, hakuna aliyeweza kutafsiri ile ndoto. Mfalme aliamuru wenye hekima wote wauawe kwa sababu walishindwa kutafsiri ndoto ya mfalme. 

Waliotakiwa kuuawa walipewa taarifa, ndipo katika somo la leo asubuhi tunamuona Daniel akiwaambia wenzake waombe rehema ya Mungu kwa habari ya ndoto ile. Katika sala zao ndipo Danieli alipofunukia maana ya ndoto ya mfalme. Ukiendelea kusoma unaona Danieli akitafsiri ndoto mbele ya mfalme, hadi mfalme alimsujudia Danieli!

Danieli 2:46

Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danielii, akatoa amri wamtolee Danielii sadaka na uvumba.

Danieli aliweza kutafsiri ndoto kwa msaada wa Mungu.

Sisi leo tunaweza kufanikiwa katika kazi zetu kwa njia ya Yesu Kristo. Yesu anapojifunua kwetu anatupa uhakika kwamba ni kweli alifufuka, ni yule yule. Anatuita kubaki kwake tukimtumikia na kumtegemea kwa siku zote za maisha yetu.

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.

 

Heri Buberwa