Date: 
24-04-2023
Reading: 
Isaya 40:10-11

Hii ni Pasaka 

Jumatatu asubuhi tarehe 24.04.2023

Isaya 40:10-11

10 Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake.

11 Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Yesu Kristo ni mchungaji mwema;

Unabii wa Isaya uko katika vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kabla ya uhamisho. Wakati huu ndipo Isaya alipoitwa. Israeli na Yuda zilikuwa katika msukosuko kisiasa. Mataifa makubwa yalikuwa karibu kuwavamia. Watu walipanga jinsi ya kutafuta misaada kwa ajili ya vita, lakini Isaya aliikataa mipango hiyo. Isaya alikaza kumwamini na kumtegemea Mungu, akisema kutegemea mataifa ni kujiangamiza mwenyewe (sura ya 1 hadi 39)

Kipindi cha pili Wayahudi waliouwa uhamishoni Babeli. Wakati huu walikuwa kwenye masikitiko na kukata tamaa.Nabii anatuliza mioyo ya wafungwa huko Babèli (40:1). Anatangaza kuwa Mungu atawapa uhuru na kuwarudisha katika nchi yao. Yote haya yatawezekana kwa nguvu ya Bwana (40-55)

Kipindi cha tatu ni baada ya kutoka uhamishoni. Wayahudi waliporudi toka Babeli waliona hatma yao haipo, lakini Nabii anawatia moyo na kuwapa matumaini ya hali njema zaidi hapo baadaye (56-66)

Baada ya utangulizi huo, soma tena somo letu;

Isaya 40:10-11

10 Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake.
11 Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Unaona kwamba somo la asubuhi hii ni kipindi cha pili, ambapo Wayahudi walikuwa uhamishoni Babeli. Walikuwa kwenye masikitiko makubwa. Walikata tamaa bila ya kuwa na tumaini. Ndipo tumesoma Bwana akituma ujumbe kuwa atawaendea kama shujaa kuwaokoa. Bwana anatangaza kuwaendea kama Mchungaji wao na kuwatunza. Anaahidi kutowaacha. Na kama tulivyoona, baadaye waliondoka uhamishoni na kurudi kwenye nchi yao. Kumbe alitimiza ahadi yake kwao, aliwaendea, akawaokoa, na kuwatunza kama Mchungaji wao.

Mungu hakuwahi kuwaacha watu wake, ndiyo maana alimtuma Yesu Kristo kuja kwetu akatuokoa kwa njia ya kifo msalabani na kufufuka. Leo Yesu anajitambulisha kwetu kama Mchungaji mwema, aliyejitoa kwa ajili yetu. Ni wajibu wetu kukaa zizini na kumsikiliza yeye aliye Mchungaji wetu mwema, sasa na siku zote. Amina.

Tunakutakia wiki njema.

Heri Buberwa Nteboya