Date: 
27-05-2025
Reading: 
Mwanzo 45:21-24

Hii ni Pasaka;

Jumanne asubuhi tarehe 27.05.2025

Mwanzo 45:21-24

21 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani.

22 Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili.

23 Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani.

24 Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.

Ndugu wakae pamoja kwa umoja;

Msingi wa somo la asubuhi hii;

Yusufu hakupendwa na kaka zake kwa ambavyo Yakobo baba yao alimpenda. Hivyo siku moja wakiwa malishoni wakapanga wamuue, Rubeni akakataa, baada ya mjadala mrefu wakamuuza kwa Waishmaeli ambao baadae walimuuza kwa Wamisri. Huko Yusufu alipitia shida nyingi lakini baadaye akaja kuwa kiongozi mkubwa chini ya Farao. Ilitokea shibe miaka 7, ikaja njaa miaka 7. Siku moja watoto wa Yakobo walifuata chakula Misri, ndipo Yusufu akawapa chakula na kuwaambia "msigombane njiani". 

Kinyume cha kugombana ni kupatana. Kwa hiyo Yusufu alikuwa anawausia ndugu zake wakae kwa kupatana. Kupatana kunahitaji kuonana hadharani na kuambiana ukweli bila kujali maumivu. Kupatana ni matendo, na siyo maneno tu. Tuepuke migawanyiko inayotugawa tusikae pamoja. Tusameheane na kuonyana kwa upendo, ili ufalme wa Mungu uenezwe popote kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa