Date: 
07-07-2025
Reading: 
Mithali 5:1-7

Jumatatu asubuhi tarehe 07.07.2025

Mithali 5:1-7

1 Mwanangu, sikiliza hekima yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu;

2 Upate kuilinda busara, Na midomo yako iyahifadhi maarifa.

3 Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;

4 Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni mkali kama upanga wa makali kuwili.

5 Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu;

6 Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.

7 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala msiache maneno ya kinywa changu.

Msingi wa uongozi bora;

Kijana Mkristo ni chachu ya maendeleo;

Sura ya 5 ya kitabu cha Mithali ni maonyo juu ya hatari ya uzinzi, na wito wa uaminifu katika ndoa. Mfalme Suleimani anatumia lugha kali kuelezea njia za majaribu na madhara yake katika Taifa la Mungu. Suleimani anaonesha malaya (asiye mwaminifu) afanyavyo kutenda dhambi, akielekea kuikosa njia ya uzima, na njia yake ni kutangatanga. 

Mkazo wa Suleimani ni kuishika hekima ya Mungu ambayo hupatikana kwa njia ya neno lake. Anaendelea kuandika kwamba mwisho wa dhambi ni mchungu, ni mkali kama upanga ukatao kuwili. Suleimani ametumia lugha ya malaya kuonesha wasio waaminifu katika nyumba zao, lakini kwa tafakari ya wiki hii naweza kusema tunaalikwa kuwa waadilifu na waaminifu katika kazi zetu. Imani yetu inatutuma kutenda yote kwa uaminifu ili kuujenga mwili wa Kristo. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa