
Siku ya Jumapili, tarehe 26/10/2025, Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front uliadhimisha kilele cha Sikukuu ya Mavuno ya Mwaka 2025, maadhimisho ambayo hufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa washarika kumtolea Mungu sehemu ya matunda au mavuno ya kazi walizozifanya kwa kipindi cha mwaka mzima.
Ibada ya kusherehekea sikukuu hii ya mavuno kwa mwaka huu imefanyika katika viwanja vya usharika wa Kanisa Kuu Azania Front ikihudhuiriwa na mamia ya washarika waliojitokeza wakiwa sadaka za mavuno tayari kwa kumtolea Mungu.
Ibada hiyo imeongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye Pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Baba Askofu Dkt. Alex G. Malasusa akiwa pamoja na Msaidizi wa Askofu Dean Chediel A. Lwiza, Mch. Victor Makundi na Mch. Joseph Mlaki; wakisaidiwa na Watumishi wote wa Usharika pamoja na Wazee wa Kanisa.
Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa aliwakumbusha washarika wa Azania Front kuwa Sikukuu ya Mavuno ni siku muhimu sana katika maisha ya kikristo. Baba Askofu aliwaambia washarika kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kodi na sadaka na kwamba sadaka hutolewa kwa hiari na kwa uaminifu mkubwa sana.
“Ndugu zangu, sadaka kanisani sio kodi na ndiyo maana huwezi kughushi sadaka. Sadaka ni wewe na Mungu wako,” alisema.
“Kama kuna sadaka haihitaji kulazimishwa ni mavuno kwasababu wewe ndiye unajua ni jinsi gani Mungu amekubariki, amekuheshimisha na kukupitisha katika maeneo ambayo hata wewe unashangaa umewezaje kupita. Sikukuu hii ndugu zangu ni sikukuu inayotupa fursa ya kuonyesha ukarimu wetu kwa Mungu”, alisema.
“Tujifunze kutoa kwa sababu apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu lakini apandaye haba atavuna haba. Katika somo hili tumekumbushwa tusitoe kwa kulazimishwa bali tutoe kwa hiari. Mungu akubariki sana, abariki sadaka ambayo leo umeitoa lakini sadaka kubwa ambayo Mungu anaitaka leo uitoe ni kuutoa moyo wako kwake, na hapo ndipo wengi tunapofeli kwa sababu wengi tunadhani Mungu anahitaji fedha. Mungu hahitaji fedha kwa sababu fedha na dhahabu zinatoka kwake, anachokihitaji ni moyo wako tu”, alisema Baba Askofu kwa msisitizo wakati akihitimisha mahubiri yake.
Ibada ya sikukuu ya mavuno ilitanguliwa na maandamano mafupi na utoaji wa sadaka pamoja na mavuno huku ikihitimishwa kwa mahubiri kutoka kwa Baba Askofu Malasusa na mwisho kabisa ukifanyika mnada wa bidhaa au mavuno yaliyokuwa yamewasilishwa na washarika.
Katika hatua nyingine, Kwaya ya AIC Neema Gospel Choir ya jijini Dar es Salaam iliungana na Kwaya za Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front katika kuipamba sikukuu hiyo kupitia tungo mbalimbali za kumtukuza Bwana Mungu wetu.
Angalia picha zaidi hapa chini:

Picha: AZF Media Team
Tazama ibada hiyo hapa: https://www.youtube.com/watch?v=gh6zc08aXrk&t=2991s
------- #### -------
