Date:
07-08-2025
Reading:
Mwanzo 41:46-48
Alhamisi asubuhi tarehe 07.08.2025
Mwanzo 41:46-48
46 Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri.
47 Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi.
48 Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake.
Tunaitwa kuzaa matunda mema;
Farao aliota ndoto ambayo hakuielewa, akaletwa Yusufu aliyekuwa mfungwa gerezani akaitafsiri. Kwa tafsiri ya Yusufu, ndoto ya Farao ilihusu miaka saba ya shibe ndani ya Misri na miaka saba ya njaa. Mfalme alitakiwa kutafuta usimamizi katika nchi, ambapo chakula kingekusanywa wakati wa shibe, ili wakati wa njaa kuwe na chakula cha kutosha. Baada ya Yusufu kutafsiri ndoto, Farao alifurahi sana na kumfanya kiongozi mkubwa juu ya Misri baada ya Mfalme.
Baada ya kufanywa mkubwa akimfuatia Farao katika Misri,Somo linaonesha Yusufu akikusanya chakula cha kutosha wakati wa shibe. Chakula hiki ndicho kilikuja kuwasaidia watu wasife njaa wakati wa miaka saba ya njaa, wakiwemo ndugu zake. Kwa tafakari ya wiki hii, naweza kusema Yusufu alimzalia Bwana matunda kwa nafasi yake. Tunakumbushwa kumzalia Bwana matunda, kila mmoja kwa nafasi yake. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650