Date:
11-08-2025
Reading:
Mithali 18:18
Jumatatu asubuhi tarehe 11.08.2025
Mithali 18:18
Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu.
Uchaguzi wa busara;
Mithali tunayosoma asubuhi ya leo inaongelea jinsi ya kutafuta suluhu katikati ya migogoro na mashindano katika jamii ya wakati ule. Ni njia ambayo ilitumika na watu kufanya maamuzi kulipokuwa na hoja tofauti. Kupiga kura ilikuwa ni njia ya kawaida kwa uamuzi, au kugawana vitu kwa usawa. Njia hii ilisaidia kuondoa mihemko, hisia na upendeleo, ambapo watu waliweza kuamua kwa pamoja na kuamua pasipo kuumiza upande wowote.
Katika maisha ya tunayoishi, tunazo tofauti miongoni mwetu. Badala ya kuongea sana, tunazo njia za kufanya maamuzi kwa kufuata taratibu za sehemu husika. Yaweza kuwa katiba, kanuni, sheria, au vinginevyo kulingana na makubaliano ya wahusika. Siku zote lengo siyo mtu au upande kushinda, bali kuamua kwa ajili ya kutatua jambo fulani.
Kwa hiyo tunachokiona ni watu wakaao pamoja na kufanya uamuzi wa pamoja kwa ajili ya kwenda pamoja katika umoja wao. Kura imetumika kama dhana ya kufanya maamuzi. Kumbe tunaelekezwa kufanya maamuzi sahihi katika maisha yetu kwa kija jambo. Uamuzi sahihi ni kumchagua Yesu Kristo awe Mwokozi wetu siku zote za maisha yetu, hata uzima wa milele. Amina
Tunakutakia wiki njema yenye uchaguzi wa busara.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650