Date: 
01-10-2025
Reading: 
Yohana 4:46-54

Jumatano asubuhi tarehe01.10.2025

Yohana 4:46-54

46 Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu.

47 Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.

48 Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?

49 Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu.

50 Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia.

51 Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai.

52 Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha.

53 Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.

54 Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

Tuwapende na kuwajali watoto katika Bwana;

Asubuhi ya leo tunamsoma ndugu aliyetoka Kapernaumu kwenda Galilaya akimfuata Yesu. Ndugu huyu alimwendea Yesu kumsihi aende kwake kumponya mwanae maana alikuwa karibu na kufa. Yesu alimuuliza kwamba bila ishara hawezi kuamini? Yule ndugu akaendelea kumuomba Yesu aende nyumbani kwake kumponya mwanae. Yesu akamtangazia uponyaji wa mtoto wake, na alipofika nyumbani akamkuta mtoto wake amepona.

Inawezekana yule ndugu alikuwa ametafuta tiba ya mtoto wake bila mafanikio, labda ndiyo maana mtoto alikaribia kufa. Lakini pia inaonesha imani ya yule ndugu, aliamini kwamba ni Yesu pekee angeweza kumponya mwanae. Baba alisafiri mbali kwa ajili ya mtoto wake mgonjwa. Inatukumbusha kupenda na kutunza familia zetu. Tuwapende na kuwajali watoto katika Bwana. Amina

Jumatano njema 

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com