Date:
23-01-2026
Reading:
Waefeso 5:23-39
Hii ni Epifania
Ijumaa asubuhi tarehe 23.01.2026
Waefeso 5:29-33
29 Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.
30 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.
31 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.
32 Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.
33 Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.
Nyumba zetu hubarikiwa na Mungu;
Mtume Paulo anaandika jinsi Kristo anavyolipenda Kanisa lake, akitoa mfano wa mtu aupendavyo mwili wake. Ni kweli tunaipenda miili yetu. Hatupendi kuwa wachafu. Paulo anatoa mfano wa miili yetu, kwa maana sisi tu viungo vya mwili wa Kristo, hivyo anatupenda upeo.
Anapotumia mfano wa mwili kuongelea Kristo na Kanisa,ni mstari wa 31 ambao pia ameutumia kwenye 1Kor 6:16, Yesu akiutumia mara kadhaa kwenye Mt 19:5, Mk 10:8 ananukuu neno la Mungu wakati ule wa uumbaji;
Mwanzo 2:24
Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.Mtume Paulo anatumia nukuu hiyo kuonesha nafasi ya mwili katika kuunganisha watu, kuwa ni upendo katika Kristo. Hivyo katika mtazamo wa Kanisa, Kristo anatupenda kuliko nafasi ya miili yetu. Upendo wake hauelezeki. Ni katika upendo huo yeye hubariki nyumba zetu.
Mtume Paulo pia anatufundisha juu ya waume kuwapenda wake zao kama Kristo alivyolipenda Kanisa hadi kulifia, na wake kuwatii waume zao maana waume ndio vichwa vya wake kama Kristo alivyo kichwa cha Kanisa. Maisha ya namna hii huleta utengemano kwenye familia, na ndipo Mungu hubariki nyumba zetu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
Mlutheri
