Event Date: 
12-08-2022

Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azania Front Cathedral mnamo tarehe 3 Julai 2022 ulifanya Harambee kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Kiharaka. Harambee hiyo iliyolenga kukusanya milioni 300 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa Kiharaka iliongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk. Alex Malasusa.

Akizungumza katika ibada hiyo maalum ya Harambee, Baba Askofu alisema kuwa hakushangazwa na namna watu wachache waliojitokeza kushiriki katika ibada hiyo. Alitoa wito kwa washarika kuacha kasumba ya kutohudhuria ibada mara wanaposikia kutakuwa na mchango kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kanisa.

“Najua katika jambo la ki-Mungu kama hili sio wote wanaweza kujitokeza, nakumbuka ilipofika saa mbili Chaplain akawa ananiambia naona watu ni wachache tusubiri waongezeke kidogo, na mimi nikamwambia hao waliokuja ni hao hao kwa sababu ki-Mungu, walioitwa ni wengi lakini wateule ni wachache, nasisi tulioko hapa leo ndio wateule ukiondoa wale ambao wapo vitandani wanaumwa,” alisema Baba Askofu. 

Katika hatua nyingine Baba Askofu aliwaasa washarika kutokata tamaa bali waendelee kujitolea na kutoa michango mbalimbali ili mradi huo upate kukamilika. “Kiroho, mradi ulioanza alafu ukakaa bila kukamilika unaleta mashaka kwa sababu Biblia inatwambia kuwa kabla ya kujenga nyumba kaa chini uhesabu gharama. Hivyo tusikate tamaa, twende mbele na Mungu atatuwezesha,” alisema Baba Askofu.

-----------------------------------

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa wa Ibada ya Harambee ya Kiharaka iliyofanyika katika viwanja vya Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral.