Jumamosi asubuhi tarehe 11.05.2024
Waefeso 1:15-23
[15]Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote,
[16]siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu,
[17]Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;
[18]macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;
[19]na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;
[20]aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;
[21]juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
[22]akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
[23]ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
Kristo amepaa katika Utukufu wake;
Asubuhi hii tunaisoma Sala ya Mtume Paulo akiwaombea Waefeso, anawaombea hekima ya Mungu ili wamjue yeye, na macho yao yatiwe nuru waweze kutambua uwezo na ukuu wa Bwana.
Ni sala ya kuwaombea,
lakini yenye mausia ya kumcha Bwana Yesu Kristo, aliyekufa na kufufuka kwa ajili yao.
Huyu ndiye Yesu Kristo aliyepaa mbinguni, anayetuita hata sasa kumfuata milele yote. Tunapotafakari sala hii, tujazwe tumaini kuwa Yesu Kristo amepaa lakini yuko nasi, hajatuacha. Wajibu wetu ni kuendelea kumfuata na kumtii, tukijua kuwa atarudi kwa hukumu ya haki kwa wote. Jumamosi njema.
Heri Buberwa