Date: 
19-08-2024
Reading: 
1 Samweli 17:5-58

Jumatatu asubuhi tarehe 19.08.2024

1 Samweli 17:51-58

51 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.

52 Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka ufikapo Gathi, na mpaka malango ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu, mpaka Gathi, na mpaka Ekroni.

53 Kisha wana wa Israeli wakarudi kutoka katika kuwafukuza Wafilisti, wakateka nyara marago yao.

54 Naye Daudi akakitwaa kichwa chake yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu; lakini silaha zake akaziweka hemani mwake.

55 Basi Sauli, hapo alipomwona Daudi akitoka ili kumwendea yule Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, Je! Abneri, kijana huyu ni mwana wa nani? Abneri akamjibu, Ee mfalme, kama iishivyo roho yako, mimi siwezi kusema.

56 Basi mfalme akasema, Uliza wewe, kijana huyu ni mwana wa nani.

57 Hata na Daudi alipokuwa yuarudi kutoka katika kumwua yule Mfilisti, Abneri alimtwaa, akamleta mbele ya Sauli, naye anacho kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake.

58 Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.

Nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari;

Sura ya 17 inaandika habari za Daudi na Goliathi. Goliathi alikuwa tishio kwa Israeli. Ilifikia hatua akawaambia watoe mtu ambaye angepigana naye, na kwamba Goliathi kama angemuua huyo mu-Israeli, basi Israeli wangekuwa watumishi wa Wafilisti. Na kama huyo mtu wa Israeli angemuua Goliathi, basi Wafilisti wangekuwa watumishi wa Israeli.

Angalia Goliathi alivyowaambia Israeli;

1 Samweli 17:8-9

8 Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi.
9 Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.

Goliathi alikuwa mtu wa vita, hivyo aliogopeka sana na watu wote. Watu wengi akiwemo Mfalme Sauli walimsihi akae mbali na Goliathi, lakini kwa ujasiri Daudi akasema angemkabili Goliathi. Daudi alirejea historia yake ya kumuua Simba machungani, kwamba Mungu aliyemuokoa katika makucha ya Simba angemuongoza kumpiga Goliathi. Daudi anaonesha kumtegemea Bwana anapoenda kumouga Goliathi;

1 Samweli 17:44-45

44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.
45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.

Kwa dharau sana, Goliathi akamjia Daudi tayari kumpiga, lakini Daudi akaweka jiwe kwenye kombeo na kumpiga yule Mfilisti usoni. Kwa hiyo Daudi akamuua Goliathi kwa jiwe, bila upanga!

Somo lenyewe;

Somo linaonesha Daudi baada ya kumuua Goliathi akimkata kichwa na kukileta Yerusalemu. Wafilisti walipoona shujaa wao ameuawa walikimbia! Bila shaka ulikuwa ni mwanzo wa harakati za kutokuwa watumishi wa Israeli kama Goliathi alivyoahidi Mwanzo.

Tunajifunza nini?

1. Goliathi aliamini katika nguvu na ubabe. Lakini kama tulivyoona katika mstari wa 45, Daudi alimtegemea Bwana kumpiga Goliathi. Kumbe maisha yetu yafaa tukimwamini Yesu na kumtegemea daima.

2. Mstari wa mwisho (58) Daudi anaulizwa na Sauli yeye ni nani? Anajibu kwamba ni mtoto wa Yese, mtumishi wa mfalme. Soma tena mstari huu;

1 Samweli 17:58

Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.

Kumbuka Daudi alikuwa amekwisha kupakwa mafuta na Samweli kuwa Mfalme (sura ya 16) lakini hakujibu kuwa ni Mfalme, bali mwana wa Yese. Daudi anaonesha unyenyekevu mbele ya Mfalme Sauli ambaye alitaka kumuua baada ya kukataliwa kuwa Mfalme. Unyenyekevu hutuweka karibu na Kristo, maana ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa. Amina

Tunakutakia wiki njema yenye Unyenyekevu 

 

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com