Hii ni Epifania
Jumatano asubuhi tarehe 05.02.2025
Matendo ya Mitume 26:24-31
24 Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili.
25 Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.
26 Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.
27 Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.
28 Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo.
29 Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.
30 Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama;
31 hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.
Mungu ni mlinzi wetu;
Ni habari ya mashtaka ya Mtume Paulo aliyotengenezewa ili auawe na Injili ya Kristo isiende mbele. Pamoja na mashtaka kusukwa na kupangiliwa ilivyotakiwa, hatma ya mashtaka yale haikuwa kama ilivyotarajiwa. Kwa mashtaka yale Paulo aliteseka katika magereza ya Kirumi mikononi mwa Wayahudi, lakini alivumilia yote akijua yupo Yesu Kristo pamoja naye.
Sasa Paulo yuko mbele ya mfalme Agripa akijitetea kwa kirefu, kwa uwazi, bila woga. Ndipo tunamsoma Liwali Festo akidakia na kumwambia Paulo kuwa ana wazimu! Baadaye wote waliokuwa barazani waligundua ya kuwa Paulo hakutenda jambo la kusababisha afungwe!
Matendo ya Mitume 26:30-31
30 Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama; 31 hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.Katikati ya mashtaka yaliyolenga Paulo afungwe, Mungu alikuwa naye, akayapangua mashtaka yake. Kwa mambo yote tunayopitia katika safari yetu ya utume na maisha kwa ujumla, Mungu ndiye mlinzi wetu. Tukae kwake daima. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa