Jumatano asubuhi tarehe 04.06.2025
Kutoka 17:8-16
8 Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu.
9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu.
10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima.
11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.
12 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.
13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.
14 Bwana akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.
15 Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi;
16 akasema, Bwana ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.
Mungu husikia maombi yetu;
Israel wakiwa bado Refidimu, baada ya kupata maji, Wamaleki walitokea kupigana na wana wa Israeli. Ikawa Musa alipoinua mkono wake Israeli walishinda, na alipoushusha mkono wake Wamaleki walishinda. Lakini Haruni na Huri walienda mbele kwa kuitegemeza mikono ya Musa, bado Israeli waliwashinda Wamaleki.
Tunaona kuwa Mungu alimtumia Musa kuwashinda Wamaleki, maana alimtegemea Bwana. Kumbuka Musa ndiye aliyemlilia Bwana Israeli walipokosa maji, Bwana akajibu. Hivyo Bwana aliendelea kumwezesha Musa maana alimtegemea.
Pamoja na kuwa mteule, Musa bado alijiona tegemezi kwa Bwana. Sisi tunao wokovu, lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa tunamtegemea Bwana. Ili tuweze kutumika kwa ukamilifu shambani mwa Bwana, tuendelee kumtegemea yeye tukiomba neema yake isipunguke kwetu wakati wote. Tunamhitaji Bwana atuwezeshe ili tuweze kutenda yatupasayo. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa