Date: 
07-06-2025
Reading: 
Yohana 7:25-32

Jumamosi asubuhi 07.06.2025

Yohana 7:25-32

25 Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue?

26 Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo?

27 Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.

28 Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi.

29 Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.

30 Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

31 Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu?

32 Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate.

Mungu husikia maombi yetu;

Pamoja na Yesu kuhubiri, kufundisha akitenda ishara nyingi, bado wapo ambao hawakumuamini. Hii inaonekana katika mstari wa kwanza kabisa wa somo hapo juu, ukionesha kwamba wapo waliotaka kumkamata Yesu ili akauawe. Lakini Yesu ndipo alizidi kupaza sauti yake hekaluni akifundisha kuwa yeye ni Mwokozi aliyetoka mbinguni. Kumbe bado kulikuwa na waliokuwa na mioyo migumu, maana pamoja na Yesu kufundisha hekaluni, bado walitafuta kumkamata! 

Msingi wa tafakari ya somo la asubuhi ya leo ni Yesu kufundisha, katikati ya umati ambao pia walikuwepo wasiomuamini. Ujumbe unaotujia ni kumuamini Yesu kwa njia ya neno lake. Hatuna haja ya kuwa na shaka, maana yeye ndiye kweli aliyetoka mbinguni kama tunavyosoma mstari wa 28. Tudumu katika Kristo aliye kweli na uzima, yeye asikiaye maombi yetu. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa