Date: 
13-06-2025
Reading: 
Matendo ya Mitume 2:14-21

Hii ni Pentekoste 

Ijumaa asubuhi tarehe 13.06.2025

Matendo ya Mitume 2:14-21

[14]Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.

[15]Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

[16]lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,

[17]Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.

[18]Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.

[19]Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi.

[20]Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri.

[21]Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.

Roho Mtakatifu ni ushindi wetu;

Ni siku ya Pentekoste, Roho anashuka, na wale mitume wanatokewa na ndimi za moto na kunena kwa lugha za wengine, hadi mkutano kushangaa!

Ndipo katika somo la leo asubuhi, Petro anasimama na kuanza kuhutubia mkutano, akiwaambia wasidhani mitume wamelewa, maana ilikuwa mapema bado. Mstari wa 14 hadi wa 36 ni hotuba ya Petro siku ile ya Pentekoste. Yapo mambo ya kuangalia japo kwa kifupi.

1.Mitume walinena lugha nyingine kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Hapa Mungu alikuwa anajidhihirisha, maana ndipo Kanisa lilikuwa linazaliwa. Mungu alikuwa anatangaza kuwa Kanisa halitakuwepo bila Roho Mtakatifu. Sisi kama Kanisa lazima tuendelee kujazwa Roho Mtakatifu wakati wote, ili Kanisa lisiyumbe.

2.Neno la Mungu ndilo linalookoa. Mitume waliponena kwa lugha, hakuna aliyempokea Yesu, walibaki kushangaa. Petro akahubiri (mst 14 hadi 36), baada ya mahubiri watu wakampokea Yesu;

Matendo ya Mitume 2:37-38

[37]Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Hivyo linalookoa ni neno la Mungu. Kunena kwa lugha na mambo mengine havimuokoi mtu, bali neno la Mungu. Sisi kama Kanisa tunao wajibu wa kusoma neno la Mungu, lakini kukazia mafundisho ya neno la Mungu katika familia, jumuiya na jamii kwa ujumla. 

3.Petro anatangaza unabii ya Yoeli kutimia.

Yoeli 2:28-29

[28]Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
[29]tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.

Huu ni uthibitisho kuwa ahadi za Mungu ni amini. Ahadi ya Mungu ilitimia kwa kumimina Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste. 

Mungu ameahidi kuwa nasi maishani. Ahadi hii ni ya kweli, inaishi. Tutadumu katika ahadi hii kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Nakutakia Ijumaa njema.

 

Heri Buberwa Nteboya