Ijumaa asubuhi tarehe 05.09.2025
Yeremia 26:1-6
1 Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa Bwana, kusema,
2 Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
3 Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.
4 Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
5 kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
6 basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.
Mungu huwapinga wenye kiburi;
Yeremia alitoa ujumbe wa Bwana kwa watu wake kuacha njia mbaya ili asiwahukumu kwa sababu ya uovu wa matendo yao. Ujumbe wa Yeremia ulikuwa kwamba watu wasipomsikia na kumcha Bwana, mji wao ungefanywa kuwa laana. Haikuwa kazi rahisi kwa Yeremia, maana kwa lugha ya leo naweza kusema walimteka. Soma hapa chini;
Yeremia 26:8-9
8 Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote Bwana aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa. 9 Kwa nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.Lakini Yeremia hakukata tamaa, alikazia ujumbe wake akiwaita wale watu kutengeneza njia zao ili kuiepuka hasira ya Mungu (13-15).
Tunaona watu wakipelekewa ujumbe, badala ya kupokea ujumbe wa Bwana wanahangaika na aliyeleta ujumbe! Tuachane na njia zetu zinazotutoa kwa Bwana. Tukishike neno lake siku zote za maisha yetu. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650