Date: 
16-09-2025
Reading: 
Ruthu 2:1-10

Jumanne asubuhi tarehe 16.09.2025

Ruthu 2:1-10

1 Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi.

2 Naye Ruthuu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda.

3 Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki.

4 Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, Bwana akae nanyi. Nao wakamwitikia, Bwana na akubariki.

5 Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani?

6 Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu;

7 naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo.

8 Basi Boazi akamwambia Ruthuu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu.

9 Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana.

10 Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni?

Mtendee mema jirani yako;

Mtu mmoja aliyeitwa Elmeleki aliondoka toka nchi ya Yuda kwa sababu ya njaa akaenda kuishi Moabu. Aliondoka yeye na mke wake aliyeitwa Naomi, na watoto wake wawili walioitwa Maloni na Kilioni. Wakiwa huko, hao watoto wawili wa kiume kila mmoja wao alioa. Elmeleki alifariki, na baadaye watoto wawili walifariki pia. Kwa hiyo Naomi akabaki na wakwe zake tu, Orpa na Ruthu. Naomi alisikia kwamba kule kwao Bethlehemu ya Yuda njaa ilikuwa imekoma, akarudi na wakwe zake katika nchi yake, yaani akaondoka Moabu kurudi Yuda.

Somo letu linaanzia hapo; Ruthu mkwe wa Naomi aliyekuja Yuda akiambatana na mama mkwe wake anaenda kuokoka masuke katikati ya watu wa Yuda. Boazi shemeji yake Naomi alimkuta huko, na alipomfahamu akamkaribisha vizuri na kumuwekea ulinzi. Boazi anamkaribisha vizuri Mmoabu katika Yuda, yaani mgeni alikaribishwa vizuri katika nchi ya ugenini. Nawe mtendee mema jirani yako. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com