Hii ni Advent;
Jumanne asubuhi tarehe 09.12.2025
2 Wakorintho 10:1-11
1 Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu;
2 naam, naomba kwamba nikiwapo, nisiwe na ujasiri kwa uthabiti ambao nahesabu kuwa nao juu ya wale wanaodhania ya kuwa sisi tunaenenda kwa jinsi ya mwili.
3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;
6 tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.
7 Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi.
8 Maana, nijapojisifu zaidi kidogo kwa ajili ya mamlaka yetu, (tuliyopewa na Bwana, tupate kuwajenga wala si kuwaangusha), sitatahayarika;
9 nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu.
10 Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu.
11 Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo.
Changamkeni Mkombozi yu karibu;
Mtume Paulo anaitetea huduma yake ya Injili kama alivyoitwa. Katika huduma yake hiyo anasema haiwezekani kwa njia ya mwili, ni katika Bwana tu. Anawaeleza watu wa Korintho kuwa unyenyekevu katika Kristo unampa ujasiri katika huduma ya Injili, maana Kristo anamuongoza katika njia sahihi. Paulo anahimiza maneno ya nyaraka zake kuwa kwenye matendo, yaani anawataka Wakorintho kulisoma na kuliishi neno la Mungu.
Ujumbe wa Mtume Paulo ni huduma njema katika Kristo, unyenyekevu na ujasiri katika kuhubiri Injili. Paulo anasema huo ndiyo msingi wake katika utume. Ni mtazamo wangu kwamba kama Paulo anavyomtazama Kristo katika huduma yake, nasi tumtazame Kristo ili atuwezeshe kutengeneza maisha yetu tunapomuishia yeye kuelekea uzima wa milele. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
