Jumanne asubuhi tarehe 05.08.2025
Yohana 4:27-38
27 Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?
28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,
29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?
30 Basi wakatoka mjini, wakamwendea.
31 Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule.
32 Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.
33 Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula?
34 Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.
35 Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.
36 Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.
37 Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine.
38 Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.
Tunaitwa kuzaa matunda mema;
Yesu anatoka Uyahudi kuelekea Galilaya, anapita katika Samaria na kumkuta mwanamke Msamaria kisimani. Yesu alimuomba mwanamke maji, yule mwanamke akashtuka kuombwa maji na Myahudi! Yesu akaendelea kumwambia kwamba yeye ndiye maji ya uzima. Yesu akamwambia tena yule mwanamke kumleta mume wake, akajibu sina mume. Yesu akamjibu kuwa alijibu vema kwamba hana mume, maana alikuwa amekuwa na wanaume watano! Yule mwanamke akamuona Yesu kuwa nabii!
Ndipo somo linaanza kwa mwanamke kuuacha mtungi wake kisimani na kwenda mjini kutangaza habari njema za Yesu Kristo. Huku nyuma wanafunzi pamoja na kushangaa Yesu akiongea na yule mwanamke, wakamtaka Yesu ale chakula. Yesu akawaambia kuwa chakula chake ni kuyatenda yaliyo mapenzi ya Mungu. Tunajifunza nini asubuhi hii?
1. Yule mwanamke baada ya kukutana na Yesu alienda mjini kuhubiri na kutangaza habari za Yesu. Alikwenda kumzalia Mungu matunda.
2. Yesu anawatuma wanafunzi wake kuyafanya yaliyo mapenzi ya Mungu, yaani wamzalie Mungu matunda.
Nasi tunaalikwa kuitenda kazi ya Mungu kwa uaminifu, kila mmoja kwa nafasi yake tukimzalia Mungu matunda. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650