Date: 
25-08-2025
Reading: 
Yeremia 5:20-30

Jumatatu asubuhi tarehe 25.08.2025

Yeremia 5:20-30

20 Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,

21 Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.

22 Je! Hamniogopi mimi? Asema Bwana; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.

23 Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.

24 Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche Bwana, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.

25 Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.

26 Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.

27 Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali.

28 Wamewanda sana, wang'aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.

29 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?

30 Jambo la ajabu, la kuchukiza, limetokea katika nchi hii!

Haki huinua Taifa

Sura ya 5 ya kitabu cha Yeremia inaangazia hukumu ya Mungu katika Yerusalemu kwa sababu ya watu kutenda dhambi na kukosa uaminifu kwa Mungu. Yeremia alitumwa kupeleka unabii wa hukumu kwa waliotenda dhambi. Somo la asubuhi hii ni sehemu ya tangazo la Yeremia akitoa ujumbe wa Bwana kwa watu wake. Yeremia anawaita watenda dhambi "wajinga wasio na ufahamu" wasiomuogopa Mungu. Yeremia anaendelea kuwaonya juu ya ukaidi na uasi wao kwa Bwana, akisema dhambi zao ziliwazuilia wasiyapate mema.

Yeremia anatoa angalizo kwa Yerusalemu kwa njia ya swali, kwamba Bwana asiwapatilize kwa dhambi zao? (29). Huu ni ujumbe wa Yeremia kwamba kwa kumuasi Bwana, watu wangeangamia. Kwa tafakari ya juma hili, Yeremia alikuwa anahubiri katikati ya watu ambao walitenda dhambi, na kwa njia hiyo wapo watu walikosa haki zao. Hivyo Yeremia anawaita kutubu ili wayapate mema ya nchi. Asubuhi hii Yesu anaendelea kutupa wito wa kutenda haki, ili watu wote wauone Utukufu wake. Pasipo haki hakuna uzima wa milele. Amina

Uwe na wiki njema ukitenda haki.

Heri Buberwa Nteboya 

bernardina.nyamichwo@gmail.com