Ijumaa asubuhi
02.01.2026
Yohana 15:1-5
[1]Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
[2]Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.
[3]Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.
[4]Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.
[5]Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
Uso wa Bwana uende pamoja nasi;
Katika Injili ya Yohana, neno "mimi" katika somo la leo ni alama ya mzabibu kama lilivyo alama nyinginezo katika sura ya Yohana (Johannine images) katika kutambua huduma ya Yesu kwa Taifa lake;
Mimi ni mkate wa uzima (6:35)
Mimi ni nuru ya ulimwengu (8:12)
Mimi ni mlango wa zizi (10:7)
Mimi ni ufufuo na uzima (11:25)
Kabla ya uchambuzi wa somo;
Injili ya Yohana sura ya 13 hadi 17 huonekana kama "mafundisho tulivu" na mahubiri pendwa katika Injili hii.
Yesu alijua muda wake ulikuwa mfupi, hivyo aliwakusanya wanafunzi wake na kuanza kuwapa mafundisho ya mwisho, yaani hadi sura ya 17. Baadaye katika sura ya 18 ndipo anasalitiwa.
Kwa maana nyingine, mafundisho haya kwa leo tungesema wakati huu walikuwa wakihitimu mafunzo, na Yesu ndiye alikuwa mgeni rasmi. Yesu alifupisha mafundisho yake, akiwaambia wasisahau nini, akiwaambia pia ukweli waliopashwa kukumbuka. Aliwaonya juu ya mateso yaliyokuwa yanakuja, akiwaasa kuwa na Imani. Sasa katikati ya mafundisho haya, Yesu leo anafundisha kuwa yeye ni mzabibu wa kweli.
Uchambuzi wa somo;
Kama nilivyoandika hapo juu, somo la leo ni fundisho kabla ya mateso. Katika sura hizi (13 hadi 17) Yesu anawahakikishia waliomsikiliza, na Kanisa la leo kwamba hajawaacha, na wanaweza kuwa imara wakikaa kwa Yesu. Fundisho hili linavaa uhusika wa mwisho wa maisha kwa mtazamo wa Yohana (Johannine escatology) unaoelezea maisha na wokovu kuwa siyo tumaini tu, bali ahadi ya maisha kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Agano la kale linaeleza sura ya watu wa Mungu kama mizabibu;
Zaburi 80:8-16
Isaya 5:1-7
Isaya 27:2-6
Ezekieli 15:1-6
Sura ya mzabibu hapa inahusishwa na andiko la Yohana kuhusu "kukaa" (ambapo ikiunganishwa na waraka wa kwanza wa Yohana, neno "kaeni" linapatikana mara 64 kati ya 118 kwenye Agano jipya) James Boyce 2012
Kuonekana mara nyingi hivyo (yaani "kaeni) ni mkazo kwa Imani, ili tuamini katika Kristo tukikaa kwake kwa maisha ya sasa na yajayo, wenye uhakika wa kuungana naye mbinguni. Ahadi ya makao ilikwishatolewa (14:1-6) Yesu anaongelea "makao mengi" neno ambalo mara nyingi linatumika kwenye sherehe za msiba kuwapa tumaini waaminio. Lakini mkazo unakuja pale anaposema kuja kukaa kwetu (14:23). Hii siyo tu ahadi ya kwenda mbinguni, bali Ujio wa Yesu mfufuka kwa wamwaminio.
Tuendelee;
Mimi ni mzabibu wa kweli;
Neno "kweli" au ukweli linatokea mara 35 katika Yohana. Ni ufunguo wa maelezo ya mzabibu. Yesu ni mzabibu wa kweli. Kama tulivyoona hapo juu, Agano la kale linaeleza juu ya sura ya watu wa Mungu na mzabibu. Yesu anajitofautisha yeye kama mzabibu, na mzabibu unaotajwa katika Agano la kale. Katika Agano la kale, watu hawakuwa mzabibu kama Mungu alivyotaka. Lakini pale Taifa la Israel liliposhindwa, Yesu alikuja kuwa mzabibu wa kweli. Yesu anasema Baba yake ndiye mkulima. Mkulima anayetajwa hapa (vinedresser) ni zaidi ya mkulima wa kawaida. Hujua hadi asili ya mimea. Huyu ndiye Mungu ajuaye watu wake toka uumbaji, na huwaongoza maisha yao yote hadi mwisho.
Ninyi ni matawi;
Kama Yesu atokavyo kwa Baba, vilevile matawi hayawezi kufanya lolote, hadi yawe na uhusiano mzuri na Yesu mfufuka. Anaposema, Mimi ni mzabibu, na ninyi matawi, ni wazi kuwa maneno haya siyo amri wala hukumu bali ni wito na ahadi. Tafsiri ya wito huu ni kuwa mbali na Yesu hakuna mafanikio.
Kuzaa matunda;
Ahadi ya kukaa kwa Yesu siyo kwa ajili yake, au ahadi hii kuisha hivihivi. Yesu anaahidi kubadilisha maisha ya waaminio. Mizabibu hupunguzwa matawi kusafishwa. Matawi yasiyofaa hukatwa. Huu ni wito kwa Kanisa kuzaa matunda. Ni uhusiano wa lengo la Mungu na nguvu yake. Yesu anatuita kuwa wanafunzi wa kudumu, katika Utukufu.
Lolote mtakalo;
Wito wa kuzaa matunda hauwezekani kutimia kama haukufanyiwa kazi. Ahadi ya kuzaa matunda inafanyiwa kazi kwa kukaa ndani ya Yesu. Sasa katika kukaa ndani ya Yesu ndiyo tunaomba lolote tunalotaka, na Yesu hujibu.
Kama matawi, tunaalikwa kukaa kwa Yesu ambaye mzabibu wa kweli ili tuweze kuzaa matunda. Yaani tumtegemee Yesu katika mwaka huu wa 2026, ili uso wake uende pamoja nasi. Tutaweza kufanya na kutenda yatupasayo tukiwa na Yesu. Katika mwaka huu wa 2026, tusimuache Yesu. Amina
Utume mwema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
