Date: 
24-01-2026
Reading: 
Mwanzo 18:1-5

Hii ni Epifania 

Jumamosi asubuhi tarehe 24.01.2026

Mwanzo 18:1-5

1 Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.

2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,

3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.

4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.

5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.

Nyumba zetu hubarikiwa na Mungu;

Ibrahimu akiwa ameketi kwenye hema yake mchana anatokewa na Bwana, anatazama mbele yake na kuwaona wageni watatu wakiwa wamesimama mbele yake. Akawalaki kwa furaha mlangoni pake, akainama mpaka chini. Ibrahimu bila shaka alitambua ni Bwana, akaomba asimpite. Akawakirimu wageni, yakaletwa maji wakanawa miguu, wakapumzika.

Tunachosoma asubuhi ya leo ni ukarimu na utayari wa Ibrahimu kupokea wageni. Hakuwafahamu, aliwaona tu mbele ya hema yake akawakaribisha. Hii ni ishara ya upendo. Hapa Ibrahimu anatukumbusha kuishi kwa upendo, yaani tupendane, tukaribishe wageni, tutendeane wema, tupatane, lakini kubwa zaidi tumtumaini Yesu ambaye hubariki nyumba zetu. Amina

Siku njema

Heri Buberwa Mlutheri 

Mlutheri