Date: 
31-03-2023
Reading: 
Ayubu 33:13-30

Hii ni Kwaresma 

Ijumaa asubuhi tarehe 31.03.2023

Ayubu 33:13-30

13 Nawe kwani kumnung'unikia, Kwa vile asivyotoa hesabu ya mambo yake yote?

14 Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.

15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;

16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,

17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;

18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.

19 Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;

20 Hata roho yake huchukia chakula, Na nafsi yake huchukia nyama nzuri.

21 Nyama ya mwili wake huliwa, isionekane; Na mifupa yake isiyoonekana yatokea nje.

22 Naam, nafsi yake inakaribia shimoni, Na uhai wake unakaribia waangamizi.

23 Kwamba akiwapo malaika pamoja naye, Mpatanishi mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo;

24 Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi.

25 Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; Huzirudia siku za ujana wake;

26 Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; Hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejezea mtu haki yake.

27 Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea, Wala sikulipizwa jambo hilo;

28 Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, Na uhai wangu utautazama mwanga.

29 Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu,

30 Ili kurudisha roho yake itoke shimoni, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai.

Yesu ni mpatanishi;

Ayubu alipitia shida na tabu nyingi. Aliugua, akapoteza mali na familia. Kuna wakati alilalamika hadi akakosolewa na Mungu (sura ya 5). Ilifikia hatua akatoa ombi la kukata tamaa (sura 14). Lakini katikati ya yote hayo Ayubu alikiri kuwa ukuu wa Mungu hauchunguziki sura 26)

Katikati ya maelezo na maneno ya Ayubu, Somo la asubuhi hii tunamsoma Elihu akimkemea Ayubu kwa kuhoji na kulalamika baada ya kuugua. Katika somo tunaona Elihu akisema kuwa Mungu ndiye mponyaji wa wote wauguao, anamtaka Ayubu kuendelea kumuomba Mungu naye atamtakabali. Ayubu aliendelea kumtumaini Bwana, naye alimjibu (sura 38).

Mstari wa 23 unamtaja malaika wa Bwana kufanya upatanisho kati ya watu na Mungu. Mungu anaonekana kuwa na rehema katika kufanya ukombozi kwa watu wake, kama alivyomponya Ayubu.

Mungu ametuokoa kwa njia ya mwanae Yesu Kristo, ambaye alifanyika mpatanishi kati yetu na Mungu. Hatma yetu iko mikononi mwa Yesu Kristo, hivyo tukae ndani yake ili tusiangamie.

Siku njema.

 

Heri Buberwa