Date: 
24-10-2022
Reading: 
Luka 7:2-12

Jumatatu asubuhi tarehe 24.10.2022

Luka 7:2-10

[2]Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana.

[3]Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake.

[4]Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili;

[5]maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.

[6]Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;

[7]kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona.

[8]Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

[9]Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.

[10]Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.

Imani yako imekuponya;

Akida mmoja alikuwa na mtumwa wake ambaye alikuwa mgonjwa. Akida huyo alikuwa akiwasimamia askari wengine, yaani alikuwa kiongozi wao. Alikuwa na mamlaka. Japokuwa haiandikwi, lakini kuna uwezekano kuwa alikwisha mtafutia tiba mtumwa wake huyo bila mafanikio. Aliamua kutafuta msaada kwa Yesu, bila shaka baada ya kusikia habari zake.

Ni wazi kuwa akida yule alimfuata Yesu amponye mtumwa wake kwa sababu ya Imani. Pamoja na ukubwa wake kazini aliamini kuwa Yesu ndiye angeweza kumponya mtumwa wake. Aliweka Imani yake kwa Yesu, kama Yesu mwenyewe alivyosema;

Luka 7:9

[9]Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.

Tunapomshukuru Mungu kwa kutupa Juma lingine, tutafakari kama tunamfuata Yesu kwa Imani ya kweli. Tumfuate Yesu kwa kumwamini kama Mwokozi wa ulimwengu. Hivyo tunaalikwa kuwa na Imani thabiti katika Kristo, ili maisha yetu yawe yenye ushuhuda.

Nakutakia wiki njema