Date: 
27-09-2022
Reading: 
Matendo 4:13-22

Jumanne asubuhi tarehe 27.09.2022

Matendo ya Mitume 4:13-22

[13]Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.

[14]Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu.

[15]Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao,

[16]wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.

[17]Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili.

[18]Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.

[19]Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;

[20]maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.

[21]Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka;

[22]maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini.

Uchaguzi wa busara;

Matendo ya mitume sura ya 3 Petro akiwa na Yohana wakiingia hekaluni kusali, anaomba na kiwete mlangoni anapona. Ilikuwa habari kubwa. Somo la leo asubuhi ni mwendelezo wa makuhani na waandishi wakiwahoji Petro na Yohana juu ya mamlaka yao hadi kufanya ishara namna ile. Tumeona Petro na Yohana wakiambiwa wasiseme tena kuhusu Yesu (18) lakini wao wanasema hawakuwa tayari kuacha kusema habari za Yesu! (20)

Pamoja na vikwazo, kukamatwa, kuzuiwa, kutishwa n.k Petro na Yohana walishikilia kuendelea na kazi ya kuhubiri Injili. Wito unakuja kwetu asubuhi hii kuchagua kukaa na Yesu, katikati ya changamoto tunazopitia. Yesu yuko nasi wakati wote, anatuita kudumu katika ufalme wake. Ni wajibu wetu kuchagua kumfuata, tukidumu katika uchaguzi huo sasa na siku zote. Amina. 

Siku njema.