Date: 
24-06-2022
Reading: 
Mathayo 18:19-20

Ijumaa asubuhi tarehe 24.06.2022

Mathayo 18:19-20

19 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.

20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.

Msigombane njiani;

Yesu alikuwa akiwahakikishia wanafunzi wake kuwa yupo nao katika utume wao, na wakifanya kazi kwa pamoja anawasikia. Ndiyo maana anawaambia wawili wakipatana duniani, watafanyiwa na Baba. Wakikusanyika kwa jina la Yesu, atakuwa katikati yao. Hapa Yesu alionesha kuwa wafanye kazi kwa umoja katika jina lake.

Ukiendelea kusoma mbele kidogo, Petro anauliza juu ya kusamehe wanaokosa;

Mathayo 18:21-22

21 Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?
 
22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

Yesu hapa anatoa fundisho kuwa kukaa na kutumika pamoja kunawezekana kwa msamaha. Msamaha hauna kiwango, jambo la muhimu ni kusamehe kila anayekukosea, mara zote. Tukisameheana tunafanya kazi pamoja, na Mungu anakuwa katikati yetu akituepusha kugombana njiani.

Ijumaa njema.