Date: 
11-07-2023
Reading: 
2Timotheo 2:1-2

Jumanne asubuhi tarehe 11.07.2023

2 Timotheo 2:1-2

1 Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu.

2 Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.

Mtu akinitumikia na anifuate;

Mtume Paulo alimuandikia Timotheo kukaa na kudumu katika neema itokayo kwa Kristo Yesu. Akaendelea kumpa ujumbe wa kudumisha mafundisho yaliyo kweli ya Kristo. Ukiendelea kusoma unaona msisitizo wa Paulo kwa Timotheo kuwa askari wa Yesu, apigane vita bila kuchoka. Paulo hapa alimtaka Timotheo kumtumikia Yesu siku zote za maisha yake.

Ujumbe wa Mtume Paulo kwa Timotheo ni kumtumikia Yesu Kristo kwa uaminifu pasipo kuchoka, ndiyo maana Paulo anatumia dhana ya kuwa askari hodari. Katika utume huo, anamsisitiza kumwamini Yesu na kudumu katika Injili maana neno la Mungu halifungwi;

2 Timotheo 2:8-9

8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu.
9 Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.

Imani kwa Yesu Kristo ndiyo msimamo imara kwa Mkristo yeyote, na kwa imani hiyo tunaalikwa kumtumikia na kumfuata Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu. Amina.

Siku njema.

Heri Buberwa