Date: 
15-09-2023
Reading: 
2 Mambo ya Nyakati 7:1-10

1 Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba.
2 Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.
3 Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.
4 Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana.
5 Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu.
6 Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya Bwana, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama.
7 Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta.
8 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.
9 Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.
10 Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.

Uwakili wetu kwa Bwana;

Baada ya sala ndefu ya kitume aliyosali Suleimani (sura ya 6), moto ulishuka toka mbinguni ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu. Baada ya moto ule, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba yote ile kiasi kwamba makuhani hawakuweza kuingia ndani.  Suleimani aliwaongoza watu kumwabudu Bwana na kutoa sadaka baada ya kuuona utukufu ule.

Wana wa Israeli waliuona utukufu wa Mungu wakatoa sadaka. Utukufu wa Mungu kwetu upo kwa njia ya wokovu aliotupa kwa njia ya kifo cha Yesu Kristo msalabani. Na kwa sababu hii tunawajibika kutunza mali alizotupa, na kumtolea kwa ajili ya kazi yake.

Amina.

------------------------------

Heri Buberwa - Mlutheri