Date: 
23-10-2023
Reading: 
1Samweli 3:5-14

Jumatatu asubuhi tarehe23.10.2023

1 Samweli 3:5-14

5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.

6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.

7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.

9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.

10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.

11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.

12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.

13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.

14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.

Tuheshimu wito tuliopewa na Mungu;

Bwana Asifiwe;

Tunalianza juma kwa kumsoma Samweli alivyoitwa na Mungu kuingia kwenye utume. Samweli aliitwa na Mungu akawa anamwendea Eli, Eli akamwambia Samweli sijakuita. Alimwambia hivyo mara ya kwanza na ya pili. Mara ya tatu ndipo Eli akajua kuwa Samweli aliitwa na Bwana. Akamuelekeza kumuitikia Bwana. Ndipo Samweli anamuitikia Bwana kwa mstari huu maarufu;

1 Samweli 3:10

Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.

Samweli aliitika kumtumikia Bwana alipoitwa. Hii inatukumbusha na sisi kudumu katika wito wetu wa kumtumikia Mungu. Safari yetu ya Imani inahusisha wito, ambao ni kumfuata Yesu, kumwamini na kumtumikia. Kumbe Yesu anapokaa kwetu anatuita kumwamini na kumtumikia. Tuheshimu wito huu. Amina.

Tunakutakia wiki njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri