Date: 
06-01-2024
Reading: 
Yohana 8:12-14

Hii ni Epifania 

Jumamosi ya tarehe 06.01.2024

Siku ya Epifania (Ufunuo)

Masomo;

Zab 97:1-7

Isa 60:4-5

*Yn 8:12-14

Yohana 8:12-14

12 Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

13 Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.

14 Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako.

Yesu ni nuru ya ulimwengu.

Epifania ni nini?

Neno Epifania linatokana na neno la Kiyunani "epiphaneia" likimaana "udhihirisho". Ni siku ambayo wakristo huadhimisha udhihirisho wa kwanza wa Yesu kwa mataifa. Udhihirisho huu huwasilishwa na wale wataalamu wa nyota (Mt 2:1-12) walivyoifuata ile nyota ya Mashariki hadi kumuona. Pia udhihirisho huo wa kiimani ni kama ulivyotokea Yesu akibatizwa mtoni Yordani na ishara yake ya kwanza kule Kana ya Galilaya. Epifania ni mojawapo ya sikukuu tatu za zamani sana katika Kanisa, nyingine zikiwa ni Noeli na Pasaka. Kanisa Katoliki la Rumi, Makanisa mengi ya Kilutheri, Anglikana na mengine baadhi huadhimisha sikukuu hii siku ya tarehe 06 mwezi wa kwanza (kama leo), siku 12mbaada ya Noeli, wakati baadhi ya makanisa ya Mashariki ya Orthodox huadhimisha siku hii tarehe 19.01 maana wao huadhimisha Noeli tarehe 06.01. Maelezo yafuatayo yanasimulia kwa ufupi;

i) Sikukuu ya Epifania huadhimishwa tarehe 06.01 ikiwa ni alama ya kumaliza mzunguko wa "nuru" katika kalenda ya Liturjia ya Kanisa. Mzunguko huu huanza na Majilio, huendelea na Noeli, na humalizika na Epifania ambayo humaanisha udhihirisho au Ufunuo. Siku ya adhimisho huwa haibadiliki maana hufuata kalenda ya kawaida.

ii) Katika adhimisho hili, mambo matatu hukumbukwa katika Epifania ambayo ni wataalamu wa nyota kwenda kumuona Yesu (Mt 2:1-12), Ubatizo wa Yesu kwenye mto Yordani (Mt 3:1-12, Luka 3:21-22, Mk 1:1-9) na ishara ya maji kuwa divai huko Kana (Yn 2:1-11)

iii) Umuhimu wa Epifania kiTheologia ni pale Yesu alipofunuliwa kama Mwana wa Mungu, aliyefanyila mwanadamu. Yaani neno aliyefanyika mwili kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Mtume Paulo anatumia maudhui ya Epifania kueleza Yesu alivyofunuliwa kwetu na ujio wake kwa mara ya pili;

2 Timotheo 1:9-10

[9]ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,
[10]na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;

Tito 2:13

[13]tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;

2 Wathesalonike 2:8

[8]Hapo ndipo atakapofunuliwa yule mwasi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

iv) Adhimisho la kale kabisa lilifanyika huko Alexandria, Misri katika karne ya tatu. Inaaminika kuwa lilikuwa ni adhimisho la hujuma, ambapo Kanisa lililenga kukabiliana na sherehe za ''aion" mungu wa wakati ule katika Misri, sherehe ambazo zilichukuliwa kama ni za kubadilisha maji kuwa divai (Andrew Dragos, 2018)

v) Ni Injili ya Mathayo tu ambayo inawataja Mamajusi ambao wanatajwa kama wataalamu wa nyota toka Mashariki (tafsiri baadhi huwataja kama werevu, na nyingine wafalme) soma Dan 1:20; 2:2; uone majukumu yao katika mabaraza. Idadi yao haitajwi lakini hudhaniwa kuwa walikuwa wengi. Kwamba walikuwa watatu, hiyo hutajwa kwa sababu walitoa zawadi tatu, yaani uvumba, tunu na manemane kuashiria mwanadamu aliye Mungu kweli na mfalme. Maana yake Yesu alidhihirika kwao. 

vi) Mamajusi walikwenda kumuona mtoto Yesu nyumbani na siyo horini kama wale Wachungaji tuliowasoma siku ya Noeli. Hii ilitokea miaka miwili baada ya Yesu kuzaliwa. Asili ya Mamajusi haijulikani, japokuwa huonekana kuwa walitokea Peresi au Babiloni. Baadhi ya wasomi wa Agano la kale husema kuwa Mamajusi walijifunza na kupata habari za kuja kwa Mesiya kutoka kwa Wayahudi (kama anavyoandika Nabii Danieli) na waliyafahamu maandiko ya zamani (Agano la kale) ingawa hitimisho la hili siyo halisi (the evidence for this is inconclusive). Lengo hapa ni kuona Yesu alivyodhihirika kwa ulimwengu, haikuwa rahisi.

vii) Nyota zilifahamika kuwa na ishara mbaya kwa watawala. Hivyo Mfalme Herode, myahudi asiye mwaminifu kwa viwango vya wakati ule alihisi dalili mbaya kwa utawala wake. Maandiko hayaelezi nyota iliashiria nini, hoja hapa ni kuwa nyota ilikuwa njia ya Yesu kudhuhirika.

Nimeandika kwa kirefu kidogo ili upate mwanga kuhusu sikukuu hii ya Epifania, Siku ambayo tunaadhimisha jinsi Yesu alivyodhihirika kwa ulimwengu.

Sasa tukirudi kwenye somo la Epifania leo;

Yesu alikuwa Yerusalemu, wayahudi walifanya sherehe ya mahema (vibanda) ambapo Kuhani alienda kwenye kisima cha Siloam na kuchota maji na kuyaleta Altareni na kuyamwaga. Hii ilikuwa ni ukumbusho wa jinsi Mungu alivyowapa maji wana wa Israeli jangwani. Ni hapa ambapo Bwana Yesu alisema kuwa yeye ni maji ya uzima, yaondoayo kiu. (Yn 7:37-38) 

Ukiendelea kusoma sura ya 7, yaliendelea kutokea mambo kadhaa siku ya sherehe za vibanda, na ukianza kusoma sura ya 8, inaanza habari ya mwanamke mzinzi. Mbobezi wa Agano jipya, Steven J Cole anaandika kuwa habari hii ya mwanamke mzinzi haikuwa sehemu ya Injili asilia ya Yohana (was not part of John's original gospel) 

Hivyo, baada ya sherehe za vibanda, na yaliyotokea, ndipo Bwana Yesu anasema yeye ni nuru ya ulimwengu. Sidhani ilikuwa rahisi kwa wayahudi kusikia na kuamini! 

Tutafakari nuru hii;

1. Bwana Yesu anatoa dai la kushangaza kuwa yeye ni nuru ya ulimwengu;

Kuna mambo kadhaa ya kuangalia hapa;

a) Yesu anaposema kuwa yeye ni nuru ya ulimwengu, anamaanisha kuwa yeye ni Mungu.

Katika Agano la kale, wayahudi waliitambua nguzo na wingu kama Bwana;

Kutoka 13:21

[21]BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;

Soma pia Kutoka 14:19-25

Hata katika unabii wa kuja kwa Yesu inatabiriwa;

Isaya 9:2

[2]Watu wale waliokwenda katika giza 
Wameona nuru kuu; 
Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, 
Nuru imewaangaza.

Kumbe hadi hapo Yesu anaposema kuwa ni nuru ya ulimwengu, anadhihirisha kuwa yeye ni Mungu.

b) Bwana Yesu anaonyesha kweli ya Mungu kwetu;

Kama tulivyosoma mstari wa 14;

Yesu alitoka kwa Baba, na anarudi kwa Baba. Na zaidi ya hapo, yeye na Baba ni umoja;

Yohana 10:30

[30]Mimi na Baba tu umoja.

Na kila aliyemuona yeye amemuona Baba;

Yohana 14:9

[9]Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?

Yohana anaeleza pia;

Yohana 1:18

[18]Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.

Hivyo Yesu anaonyesha ukweli kuhusu Mungu Baba ukoje kwetu. Kama unahangaika kutafuta Mungu yukoje, na ni dhahiri kuwa haonekani kwa macho ya kawaida, fahamu ya kuwa hakuna aliyewahi kumuona kwa macho. Tunaweza kumjua Mungu kupitia kwake Yesu Kristo (Luka 10:22)

c) Yesu anaonyesha ukweli kuhusu sisi;

Ukweli ni kuwa sisi hatujijui, ni Yesu anayetujua. (Yoh 2:24-25). Tusipomjua Bwana, hata yasiyofaa tunayaona sawa tu. Na hili ndilo linatokea mara nyingi kwa baadhi yetu. Hivyo Yesu anapokuwa nuru ya ulimwengu, analiondoa giza linalosababisha tusienende ipasavyo, kwa kutuangazia kwa nuru yake.

Wasioamini wana giza katika uelewa wao. Wanaihitaji nuru kuwaangazia, nuru ambayo ni Yesu Kristo mwenyewe. Tunapomfuata, Yesu anaahidi kututoa gizani, na kamwe hatutembei gizani tena, tunayo nuru iletayo uzima. Yesu anatuletea nuru akijua tuko gizani.

d) Yesu anaonyesha ukweli wa Mungu kwa watu wote.

Yesu siyo nuru ya Wayahudi tu, lakini nuru ya ulimwengu wote. Wapo wanaodai kuwa na nuru ya uponyaji, wakialika watu kufuata uponyaji. Yesu ndiye nuru pekee. Wengine kwa falsafa hadi leo wanahoji uhalali wa mtu kujiita nuru! Giza nene hili! Kuitambua kweli ya nuru hii kunahitaji neema ya Mungu.

Yesu anaposema yeye ni nuru ya ulimwengu, hamaanishi kuwa watu wote kwa asili wanayo nuru hii kumfuata. Wapo walio gizani. Anatoa wito kwa wote kumfuata. Hachagui.

2. Itikio sahihi ni kumfuata Bwana Yesu kama nuru ya ulimwengu.

a) Kumfuata Yesu inamaanisha kumuamini kama Mwokozi na kumtii kama Bwana.

Huwezi kumfuata ambaye humwamini. 

Hapa tunatakiwa kujiuliza kila mmoja wetu kama tunamwamini Yesu.

Unamwamini Yesu?

Unayaamini maelezo yanayomhusu kama Mwokozi?

Unaziamini shuhuda za Mitume?

Unaamini kuwa alikufa kwa ajili ya dhambi zako?

Unaamini kuwa alifufuka?

Umaamini kuwa atarudi kwa Utukufu kuwahukumu walio hai na wafu?

Unaamini na kuzitii amri zake?

Ukimwamini katika yote haya na zaidi, hapo utamfuata kwa ukamilifu.

b) Tukimfuata Yesu kama nuru, tunayo ahadi ya kuwa naye, akitulinda na kutuongoza. 

Bwana aliwaongoza wana wa Israeli jangwani, hakuwahi kuwapungukia. Vile vile Yesu ameahidi kuwa nasi wakati wote. Tuwe ndani ya Yesu, na yeye ndani yetu;

Ujumbe mkuu hapa ni kuwa, maisha yetu hayana maana kama hatuongozwi na Bwana Yesu.

3. Itikio baya kwa Yesu ni kumkataa, tena kwa sababu za juu juu

Kama somo tulilosoma tumeona Mafarisayo wakimwambia Bwana Yesu kuwa ushuhuda wake sio wa kweli, maana anajishuhudia mwenyewe.

Hawa walimkataa Yesu hata kwa ishara nyingi, mafundisho yake, ushuhuda wa Yohana Mbatizaji na unabii katika Agano la kale uliotabiri ujio wake, kwa sababu kuwa kwa jambo lolote kuwa sahihi, lazima lishuhudiwe na watu wawili au watatu;

Kumbukumbu la Torati 19:15

[15]Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.

Lakini ukiendelea kusoma hapo tulipoishia kwa somo la leo, unaona kuwa Yesu aliwajibu kwamba hawamjui! 15-19)

Kwa kifupi Yesu anawaambia kuwa hawamjui yeye ni nani. Wanamlinganisha na taratibu zao za kawaida, wakati yeye ametoka mbinguni kwa Baba.

Kuna mambo mawili hapa;

-Wanaomjua Yesu hawamkatai

-Wanaomkataa Yesu wako gizani, wanaihitaji hii nuru ya ulimwengu, Yesu mwenyewe.

Ni wito wangu kuwa tusipende giza kuliko nuru;

Yohana 3:19

[19]Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.

Tukipenda giza tunajielezea kama waovu!

Mwisho;

Yesu anasema kuwa yeye ndiye nuru ya ulimwengu, na amfuataye hataenda gizani kamwe, atakuwa nayo nuru.

Tafakari;

Uko upande gani? Uko kwa Mafarisayo waliomkataa kama nuru kwa sababu zao za juu juu, kwa sababu huitaki nuru inayoangaza dhambi zako? Au unamfuata kwa kumwamini kama Mwokozi na kumtii kama Bwana? 

Yesu ni nuru ya ulimwengu 

Ushuhuda wake ni amini

Hima tumfuate.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com