Date: 
07-03-2024
Reading: 
Nehemia 9:30-34

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 07.03.2024

Nehemia 9:30-34

30 Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.

31 Ila kwa rehema zako nyingi hukuwakomesha kabisa, wala kuwaacha; kwa maana wewe u Mungu mwenye neema, mwenye rehema.

32 Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya, mwenye kushika maagano na rehema, mashaka yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote, tangu zamani za wafalme wa Ashuru hata leo, na yasihesabiwe kuwa ni madogo.

33 Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo mabaya;

34 na wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na baba zetu, hawakuishika sheria yako, wala hawakuzisikiliza amri zako na shuhuda zako, ulizowashuhudia.

Tumtazame Bwana aliye tumaini letu;

Nehemia sura ya 9 huitwa pia sura ya 19 ya kitabu cha Ezra-Nehemia katika maandiko ya kale ya Kiebrania ambayo hufanya Ezra na Nehemia kuwa kitabu kimoja (kumbuka Ezra hutangulia Nehemia ikiwa na sura 10). Huaminika kwamba Ezra ndiye mwandishi wa Ezra-Nehemia, pia Mambo ya Nyakati. Lakini tafiti nyingine za baadaye zilionesha kwamba mwandishi wa kitabu cha Mambo ya Nyakati ndiye mwandishi wa vitabu vyote hivi vitatu, hivyo kubaki na mtazamo uleule.

Nimeweka utangulizi huo mfupi ili nikufahamishe kuwa, sura hii ya 9 na inayotangulia (8) ni sala ya toba ya Ezra kwa ajili ya taifa la Mungu (sawa na Ezra 9-10). Mstari wa 31 katika somo unaonesha rehema za Mungu zisizokoma kwa watu wake. Katika mstari wa 33 na 34 tunaona neema na ukuu wa Mungu akitenda mema kwa watenda mabaya. Hivyo tunaiona tabia ya Kristo atendaye mema kwetu hata pale tunapokosa ushuhuda, rehema zake hazikomi. Tumtazame yeye aliye tumaini letu ili tuwe na mwisho mwema. Amina.

Alhamisi njema 

 

Heri Buberwa