Date: 
09-03-2024
Reading: 
Hesabu 21:4-9

Hii ni Kwaresma 

Jumamosi asubuhi tarehe 09.03.2024

Hesabu 21:4-9

4 Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.

5 Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.

9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Tumtazame Bwana aliye tumaini letu;

Wana wa Israeli wako safarini kutoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi. Walinung'unika jangwani kwa kukosa chakula na maji, wakamlalamikia Musa wakitamani kurudi Misri! Mungu alituma nyoka wakawauma na walikufa wengi. Hapa sasa ilibidi wamuombe Musa kuwaombea msamaha kwa Mungu, ndipo Musa akafanya nyoka wa shaba na kila aliyeitazama hata alipoumwa na nyoka aliishi.

Nyoka aliyetundikwa mtini akatazamwa na Israeli, kwa zama za Agano jipya ni Yesu Kristo aliyewambwa msalabani na kumwaga damu ili sisi tusafishwe dhambi zetu na kukombolewa kabisa. Kila aliyemtazama nyoka aliishi. Nasi tukimtazama Bwana aliye tumaini letu tunakuwa na maisha mapya, siku zote za maisha yetu. Mtazame Kristo uwe na mwisho mwema. Amina.

Jumamosi njema 

Heri Buberwa