Date: 
11-03-2024
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 32:43

Hii ni Kwaresma 
Jumatatu asubuhi tarehe 11.04.2024

Kumbukumbu la Torati 32:43
Furahini enyi mataifa, pamoja na watu wake; Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake, Atawatoza kisasi adui zake, Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake.

Furahini katika Bwana siku zote;

Bwana Asifiwe;
Neno la leo asubuhi ni hitimisho la ujumbe wa Agano la Mungu kwa Israeli baada ya kuwa wametolewa utumwani kuelekea nchi ya ahadi. Musa aliwausia kushika mafundisho ya Bwana na kulitangaza jina lake. Pamoja na kumuasi Mungu, ahadi ya Mungu kwao ilikuwa ni kutowaacha. 

Angalia Musa anavyomalizia kutoa ujumbe wa Agano la Mungu kwa Taifa lake;
Kumbukumbu la Torati 32:45-47
45 Musa akamaliza kuwaambia Israeli wote maneno haya yote;
46 akawaambia, Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo nashuhudia kwenu hivi leo; nayo waamuruni watoto wenu, wayatunze na kuyafanya maneno yote ya torati hii.
47 Kwa maana si jambo lisilofaa kwenu; maana, ni maisha yenu, na kwa jambo hili mtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki.

Hii ni baraka ambayo Musa aliwapa Israeli kabla ya kufa. 
Baada ya Musa kufa, Yoshua alivuka mto Yordan na wana wa  Israeli kuelekea nchi ya ahadi. Kumbe ahadi ya Mungu kuwa nao ilikuwa palepale.
Hata sasa, ahadi ya Mungu kwetu ni kukaa nasi na kutubariki siku zote kwa njia ya Yesu Kristo. Kristo akikaa kwetu tunashinda yote kwa jina lake. Hivyo tufurahi katika yeye atuokoaye daima. Amina.
Uwe na wiki njema 

Heri Buberwa 
Mlutheri